DKT. KALEMANI AAGIZA UJENZI WA KITUO CHA UMEME IFAKARA UANZE NDANI YA SIKU KUMI

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, amemuagiza mkandarasi, kampuni ya AEE POWER EPC S.A.U kuanza ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme katika Mji wa Ifakara ndani ya siku Kumi, ili kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Wilaya ya Kilombero pamoja na Ulanga mkoani Morogoro.

Dkt.Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 23 Februari, 2021, wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro baada ya kufika katika eneo lililotengwa kwa ajili  ya ujenzi wa kituo hicho na kubaini kuwa, kazi za ujenzi hazijaanza licha ya Mkataba kusainiwa mwezi Aprili mwaka jana.

Ad
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (katikati), akisisitiza jambo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Epanko, Wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro ambapo ameagiza kuwa migodi ya wachimbaji hao iunganishwe na umeme ndani ya Wiki Moja. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Ulanga, Mhe. Salim Almas

“Haiwezekani mkataba usainiwe kutoka Aprili mwaka jana, lakini hata msingi hamjaweka, hapa kuna uwanja tu, mi nilitaka kuja kuona kazi zinazofanyika, si uwanja, hivyo naagiza Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini , Mkandarasi na Mhandisi Mshauri wawe wameshafika katika eneo hili ifikapo tarehe 5 Mwezi ujao ili kuhakikisha ujenzi unaanza.” Amesema Dkt.Kalemani

 Waziri wa Nishati, amesema kuwa, Wilaya ya Kilombero na Ulanga zina changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa sababu zinapata umeme kutoka vituo vya Kihansi na Kidatu ambavyo vipo mbali, na kupelekea Wilaya hizo kupata umeme hafifu.

Ameongeza kuwa, jumla ya shilingi Bilioni 23 zimetolewa na Serikali ya Tanzania pamoja na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi wa kituo husika, ambacho kinapaswa kukamilika mwezi Aprili mwaka 2022.

Aidha, akiwa katika Mji wa Ifakara, Dkt.Kalemani ametoa agizo kuwa, wananchi wanaoishi katika vitongoji, vijiji na mitaa iliyo pembezoni mwa miji na inafanana na vijiji, waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu na si zaidi ya hapo.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Epanko, Wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro ambapo ameagiza kuwa migodi ya wachimbaji hao iunganishwe na umeme ndani ya Wiki Moja. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya.

Na Teresia Mhagama, Morogoro

Awali, Dkt. Kalemani alifanya ziara katika Wilaya ya Ulanga iliyokuwa na lengo la kukagua eneo la wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Epanko ili kuweza kuwapelekea nishati ya umeme itakayowawezesha kufanya uchimbaji wenye tija.

Akiwa wilayani humo Dkt. Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji hao wadogo kuanzia wiki ijayo na kwamba kazi hiyo ifanyike kwa takriban kipindi cha mwezi mmoja.

Amesema kuwa gharama ya kupeleka umeme kwenye migodi hiyo ni takribani shilingi milioni 400 ambazo zipo na kwamba wananchi hao wataunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.

Vilevile, ametoa agizo kwa watendaji wa vijiji kote nchini kuhakikisha kuwa wanatenga fedha kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye Taasisi za Umma kwenye vijiji vyao ili kuwapa wananchi huduma bora ambapo gharama ya kuunganisha umeme kwenye Taasisi hizo ni shilingi 27,000 tu.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *