Waajiri na wamiliki wa makampuni wameaswa kuzingatia sheria za kazi katika maeneo yao ya kazi ili waweze kuboresha mazingira ya utendaji kazi utakaoleta tija na ufanisi katika maeneo ya kazi.
Kauli hiyo ametolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga alipotembelea Mgodi wa almasi wa Al – Hilal Mineral Ltd uliopo wilayani Kishapu na Kiwanda cha Jielong Holding kilichopo Shinyanga Mjini kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi.
Naibu Waziri Katambi alisema kuwa ni wajibu wa waajiri kuhakikisha wanatekeleza sheria za kazi katika maeneo ya kazi akitolea mfano wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004 ambayo imekuwa ikisaidia kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyakazi na waajiri kuwa na mahusiano mazuri baina yao.
“Kwenye maeneo mengi ya kazi ambayo wamekuwa hawafuati na kutekeleza sheria za kazi migogoro hutokea mara kwa mara kati ya waajiri na wafanyakazi kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa sheria za kazi katika maeneo yao,” alieleza Katambi
“Itambulike kuwa Wajibu wa Mfanyakazi ndio haki ya mwajiri na wajibu wa mwajiri ndio haki ya mfanyakazi,” alisema
Alifafanua kuwa katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, serikali imekuwa ikifanya kaguzi na kusimamia uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi na jinsi tume ya usuluhishi na uamuzi imeendelea kutimiza wajibu wake wa kusuluhisha migogoro.
Alieleza kuwa, ushirikiano mzuri wafanyakazi na waajiri ni jambo muhimu kwa kuwa kupitia vyama vya wafanyakazi wataweza kuwasilisha malalamiko, kero au changamoto zitakazo kuwa zinawakabili katika vyombo husika na kutatuliwa.
Aliongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi ikiwemo sekta binafsi na sekta ya umma. Katika kutekeleza hayo haki imekuwa ikitolewa kwa usawa kwa waajiri na wafanyakazi kwenye maeneo yao ya kazi.
“Serikali haitasita kuwachukulia hatua waajiri ambao hawatekeleza sheria za kazi kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuamua kujichukulia maamuzi ambayo yamekuwa yakiwakandamiza wafanyakazi,” alisema Katambi
Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka waajiri wote kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi mishahara kwa wakati ili kupunguza malalamiko ya ucheleweshwaji wa mishahara. Pamoja na hayo ametoa maagizo kwa maafisa kazi kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za katika maeneo mbalimbali ya kazi iwe sekta ya umma au binanfsi.
Pia amewasihi waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati na watambue kuwa huo ni wajibu wao na ni takwa la kisheria kufanya hivyo.
Sambamba na hayo Naibu Waziri Katambi alitoa maagizo kwa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ikiwemo Idara ya Kazi, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wfanyakazi (WCF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kutoa elimu kwa umma hususan waajiri na wafanyakazi waliopo kwenye maeneo kazi ili watambue sheria za kazi, miongozo na taratibu itakayowawezesha kupata haki na ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Kwa Upande Wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko alieleza kuwa ziara hiyo ya kikazi itasaidia kuhamasisha waajiri wengi hususan wa sekta binafsi kufuata sheria za kazi na kutekeleza wajibu wao ambao utachangia kupunguza malalamiko ya wafanyakazi.