Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kushirikiana na taasisi nyengine zaidi ya taasisi wanachama wao, kueneza mafunzo na kukuza vipaji katika taasisi hizo kwa manufaa ya nchi kwa ujumla.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua na kufunga mkutano Mkuu wa tatu wa Wanawake katika Uongozi kwa mwaka 2021 na Mahafali ya 4,5,6 ya Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao leo March 04,2021 katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es salaam, ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ukuzaji wa Vipaji vya Mwanamke walio katika Uongozi ili kuwa na Mashirika Endelevu”.
Ad
”Ningependa kuona mafunzo haya yanawafikia hata viongozi wanawake walio katika Serikali yetu, Wabunge wanawake, Madiwani na hata Maafisa wengine wakuu wa Serikali ili kuhakikisha wote tunajenga mwelekeo mmoja” Amesema Makamu wa Rais
Makamu wa Rais amewahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Programu hiyo kwani imekuwa na mchango chanya katika maeneo mbalimbali ya kazi, katika jamii wakiwa kama viongozi, wananchi na pia kama Mama, Wake, Dada na washiriki wakubwa wa kujenga taifa letu.
Aidha amesisitiza kuwa pamoja na yote ya kumjenga mwanamke aweze kufikia wanapopataka, Waajiri vile vile, lazima watambue na kuiheshimu nafasi ya mwanamke pahala pa kazi na katika jamii ya Kitanzania.