Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 20 Septemba, 2021 ameshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliojadili kuhusu athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuzia juhudi za kukabiliana na janga hilo.
“Tuko katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO – 19 ambayo imeangusha sana hali ya uchumi na kufuta mafanikio yaliyokwishafikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga jamii zetu” amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza pia kuwa ingawa watu wengi wanachukulia kirahisi kupanda kwa hali ya joto kama moja ya athari za mabadiliko ya Tabia Nchi, bado hali ni ya kusikitisha kwa nchi kama Tanzania kwani hali hiyo husababisha ukame ambao ni athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo, uvuvi na misitu ambazo zinachangia 30% ya pato la Taifa na kuathiri takriban 60% ya wananchi.
Mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) utakaofanyika Glasgow, Uskochi mnamo mwezi Novemba, 2021, umejadili hatua za upatikanaji fedha kwa ajili ya kugharamia ustahimilivu na upunguzaji wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.
Washiriki katika mkutano huo pia wamejadili umuhimu wa kutilia mkazo hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia kwa kuwa athari zake na uharibifu wa mazingira hupunguza kasi ya nchi katika ukuaji kiuchumi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.
Mkutano huo ni moja ya mikutano mahsusi inayofanyika katika Kilele cha Mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa ambao kauli mbiu yake ni “Kujenga ustahimilivu kupitia matumaini – kuondokana na UVIKO – 19, kufanyia kazi mahitaji ya Ulimwengu, kuheshimu haki za watu na kuboresha Umoja wa Mataifa”.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia leo pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Comoro, Mhe. Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Rebecca Nyandeng Garang. Viongozi hao wamezungumzia kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.
Rais Samia ameelekeza kufanyika haraka kwa mikutano ya Tume za kudumu za ushirikiano baina ya mataifa hayo ili kuangalia namna ya kuboresha zaidi mahusiano.
Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amefanya mazungumzo na Mhe. Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika hilo hususan katika kusaidia wakimbizi walioko nchini Tanzania.
Filippo Grandi ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa takriban miongo sita sasa ambapo pia amependekeza kuwepo na mkutano katika ngazi ya wataalam baina ya UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa changamoto katika kuwahudumia wakimbizi.
Rais Samia ameelekeza kikao hicho kufanyika mara moja ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.