RAIS SAMIA ASHIRIKI MKUTANO WA UN KUHUSU MABADILIKO YA TABIA NCHI

Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 20 Septemba, 2021 ameshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliojadili kuhusu athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuzia juhudi za kukabiliana na janga hilo.

“Tuko katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO – 19 ambayo imeangusha sana hali ya uchumi na kufuta mafanikio yaliyokwishafikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga jamii zetu” amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Ad
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa nje ya Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa UN Jijini New York Nchini Marekani Sept 20,2021, baada ya kushiriki mkutano uliojadili masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula. Kushoto ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa New York Marekani Balozi Kennedy Gaston.

Rais Samia amesisitiza pia kuwa ingawa watu wengi wanachukulia kirahisi kupanda kwa hali ya joto kama moja ya athari za mabadiliko ya Tabia Nchi, bado hali ni ya kusikitisha kwa nchi kama Tanzania kwani hali hiyo husababisha ukame  ambao ni athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo, uvuvi na misitu ambazo zinachangia 30% ya pato la Taifa na kuathiri takriban 60% ya wananchi.

Mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) utakaofanyika Glasgow, Uskochi mnamo mwezi Novemba, 2021, umejadili hatua za upatikanaji fedha kwa ajili ya kugharamia ustahimilivu na upunguzaji wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitoka katika Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa UN Jijini New York Nchini Marekani Sept 20,2021, baada ya kushiriki mkutano uliojadili masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Washiriki katika mkutano huo pia wamejadili umuhimu wa kutilia mkazo hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia kwa kuwa athari zake na uharibifu wa mazingira hupunguza kasi ya nchi katika ukuaji kiuchumi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.

Mkutano huo ni moja ya mikutano mahsusi inayofanyika katika Kilele cha Mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa ambao kauli mbiu yake ni “Kujenga ustahimilivu kupitia matumaini – kuondokana na UVIKO – 19, kufanyia kazi mahitaji ya Ulimwengu, kuheshimu haki za watu na kuboresha Umoja wa Mataifa”.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Mhe. Rebbeca Nyandeng Garang, walipokutana Jijini New York Nchini Marekani Sept 20,2021.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia leo pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Comoro, Mhe. Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Rebecca Nyandeng Garang. Viongozi hao wamezungumzia kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Rais Samia ameelekeza kufanyika haraka kwa mikutano ya Tume za kudumu za ushirikiano baina ya mataifa hayo ili kuangalia namna ya kuboresha zaidi mahusiano.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na kuzungumza na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi UNHCR Bw. Filippo Grand, walipokutana Jijini New York Nchini Marekani Sept 20,2021.

Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amefanya mazungumzo na Mhe. Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika hilo hususan katika kusaidia wakimbizi walioko nchini Tanzania.

Filippo Grandi ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa takriban miongo sita sasa ambapo pia amependekeza kuwepo na mkutano katika ngazi ya wataalam baina ya UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa changamoto katika kuwahudumia wakimbizi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na kuzungumza na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi UNHCR Bw. Filippo Grand, walipokutana Jijini New York Nchini Marekani Sept 20,2021. PICHA NA IKULU.

Rais Samia ameelekeza kikao hicho kufanyika mara moja ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

Ad

Unaweza kuangalia pia

HERI YA SIKU YA WAFANYAKAZI, MEI MOSI

Tunawatakia Watanzania wote Heri ya Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi! Ni siku muhimu ya kuenzi …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *