Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 06 Oktoba, 2021 amezindua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma kwa niaba ya vituo vingine 5 katika mikoa mitano hapa nchini vilivyogharimu shilingi bilioni 51.53.
Vituo vingine 5 vimejengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam vituo viwili (Temeke na Kinondoni), ambapo kituo cha Temeke kitakuwa mahsusi kushughulikia mashauri ya kifamilia, mirathi, ndoa, talaka, malezi na matunzo.
Ad
Rais Samia amesema ujenzi wa kituo cha Temeke Jijini Dar es Salaam kitasaidia kupunguza mlundikano wa kesi za namna hiyo, lakini pia kitatumika kama Chuo cha kutoa mafunzo ya namna ya kushughulikia migogoro ya mirathi, ndoa, malezi na matunzo nchi nzima.
Aidha, Rais Samia ameipongeza Mahakama kwa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa Vituo Jumuishi sita vya utoaji Haki (Intergrated Justice Centres) ambao ni muhimu katika kusimamia utoaji haki nchini, kudumisha amani hususan kupitia usuluhishi wa migogoro mbalimbali inayotokea kwenye jamii pamoja na kukuza uchumi.
Amesema katika vituo hivyo kutakuwa na mahakama za ngazi zote kuanzia Mahakama ya Mwanzo, Wilaya, Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na pia eneo kwa ajili ya Mahakama ya Rufani.
Rais Samia amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kukutana na viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Wizara ya Fedha kushughulikia changamoto ya gharama ya Bandwidth ili Mahakama iweze kutekeleza majukumu yake kimalifu kupitia mfumo wa TEHAMA.
Pia, Rais Samia ameagiza Mahakama ihakikishe kuwa kwenye mpango mkakati wa miaka mitano ijayo ya maboresho ya Huduma za Utoaji Haki, mikoa 9 isiyokuwa na Mahakama Kuu ambayo ni Njombe, Geita, Singida, Manyara, Pwani, Katavi, Songwe, Lindi na Simiyu ipewe kipaumbele, zikiwemo kata na wilaya ambazo hazina Mahakama.
Vilevile, Rais Samia amewataka wadau wote wa mfumo wa utoaji haki nchini kuzingatia sheria, taratibu na kuongozwa na nafsi zao katika kufanya maamuzi ili kuwe na mafanikio yanayotarajiwa.
Rais Samia ameitaka Mahakama kushughulikia suala la ucheleweshwaji wa kesi na kumuomba Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi kuongeza usimamizi wa ubora wa maamuzi kwenye Mahakama za Mwanzo.