DKT KALEMANI ATAKA TANESCO IFANYE KAZI KAMA KAMPUNI ZA SIMU

  • Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwafuata wamiliki wa viwanda, migodi ya madini na hoteli kuwashawishi watumie umeme ili kuzalisha kwa tija hali itakayolipatia shirika hilo mapato zaidi kutokana na malipo ya umeme.
  • Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Novemba 18, mwaka huu; Waziri Kalemani alisema utaratibu huo wa kuwafuata wateja na kuwashawishi kama zinavofanya kampuni za simu, utaliongezea shirika hilo mapato hivyo litajiimarisha zaidi.
2-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) akifurahia jambo baada ya kupokea zawadi ya Kitabu maalum cha Jimbo la Musoma Vijijini kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia). Waziri alifanya ziara jimboni humo Novemba 18, 2019 na kuwasha umeme katika vijiji vya Mabui Merafuru na Kanderema.
  • Alisema, matumizi ya umeme kwa viwanda, ikiwemo migodi ya madini ni makubwa hivyo malipo yao ya umeme ni makubwa pia ndiyo maana akatoa agizo wote waunganishiwe umeme ili serikali iongeze mapato yake kupitia malipo ya umeme kutoka kwao.
  • Mbali na mapato kwa serikali, Dkt Kalemani alisema ni muhimu kwa viwanda na migodi kutumia umeme badala ya mafuta kwani inawapa unafuu mkubwa wa gharama za uzalishaji hivyo watazalisha kwa tija zaidi.
3-01
Mbunge wa Bunda Vijijini, Boniface Getere akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto kwa Mbunge), kijiji cha Bigegu, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara Novemba 18, 2019. Waziri aliwasha umeme katika kijiji hicho.
  • “Hapa Mara umeme upo wa kutosha, hakuna haja kwa wawekezaji kutumia mafuta na kutafuta kisingizio cha kutozalisha zaidi eti sababu wanatumia gharama kubwa kununulia mafuta,” alisema.
  • Waziri alitoa maelekezo kwa mameneja wa TANESCO ngazi ya wilaya na mkoa nchi nzima, kufanya tathmini ya mahitaji ya umeme kwa migodi, viwanda na hoteli kubwa kisha kuwapelekea nishati hiyo hata kama wako mbali kutoka umeme ulipo. Pia, aliagiza tathmini hiyo ihusishe kujua idadi ya transfoma zinazohitajika na kusema kwamba shirika litazigharamia.
4-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima. Waziri alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, Novemba 18, 2019 kumweleza dhamira ya ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo.
  • Awali, Mkuu wa Mkoa alimweleza Waziri kuwa wachimbaji wadogo wa madini katika Mkoa wake wanahitaji umeme ili maelekezo ya serikali kuhusu uongezaji thamani madini nchini ufanyike kwa tija.
  • Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alitembelea wilaya za Bunda na Musoma Vijijini ambapo alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika vijiji kadhaa.
5-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua miradi ya umeme vijijini, katika kijiji cha Chumwi, Kata ya Mtakuja, Musoma Vijijini, Novemba 18, 2019.
  • Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Waziri alisisitiza kuwa, wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya mwisho wa mwezi Desemba mwaka huu na kwamba serikali haitabadili msimamo wake huo.
  • Alisema, serikali imejipanga kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na umeme ifikapo Juni 2021.
6-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akisalimiana na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, alipowasili kijiji cha Kanderema, Musoma Vijijini, kuwasha rasmi umeme, Novemba 18, 2019.
  • Alitoa pongezi kwa Mbunge wa Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo na wa Bunda Vijijini, Boniface Getere kwa utendaji kazi wao mahiri hususan katika kufuatilia miradi ya umeme kwa wananchi wao na akawaahidi kuwa serikali itaendelea kufanya nao kazi bega kwa bega.
  • Kwa upande wao, Wabunge hao pia waliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi na kuwapelekea maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo umeme.
  • Katika ziara hiyo Waziri alifuatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mara, wilaya husika pamoja na kutoka wizarani, TANESCO na REA.Veronica Simba – Mara
Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWASILI WILAYANI SERENGETI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *