Na Jumbe Ismailly SINGIDA
Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya ujenzi imeshauriwa kuendelea kuwaamini Wakandarasi wazawa kuwa wana uwezo wa kujenga kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilisha kwa wakati kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.
Akitembelea na kukagua shughuli za ujenzi wa barabara pamoja na daraja la Mto Msosa zinavyoendelea kujengwa na Mkandarasi mzawa wa Kamupni ya KAGWA,Diwani Mteule wa Kata ya Ighombwe,wilayani Ikungi,Mwandu Magodi Shagembe amesisitiza kwamba endapo serikali itaendelea kuwaamini na kuwakabidhi kazi wakandarasi wazawa,itawarahisishia zaidi upatikanaji wao kutakapotokea changamoto yeyote kwenye miundombinu hiyo
“Tunaishukuru serikli ya awamu ya tano kwa kumpatia mkandarasi mzawa kazi hii ya kujenga daraja kubwa kama hili, tulikuwa hatujawahi kuona kwani tumezoea kuwaona wakandarasi kutoka Nchini China,Ujerumani lakini Tanzania sana sana wakandarasi wa kichina walikuwa wanajenga madaraja,lakini kwa serikali hii imeanza kuwaamini wakandarasi wazawa.” alisisitiza.
Aidha mwakilishi huyo wa wananchi alisisitiza pia kwamba endapo serikali itaendelea kuwaamini na kuwakabidhi kazi wakandarasi wazawa itakuwa rahisi zaidi kuwapata kunapotokea changamoto yeyote kwenye miundombinu hiyo anapohitajika kwenye eneo lake la kazi,tofauti ilivyo sasa wanapokabidhiwa wachina.
“Serikali ya awamu ya tano iendelee kuwaamini wakandarasi hawa wazawa ili waendelee kutusimamia ujenzi wetu kwa sababu wanakuwa karibu na sisi,na inakuwa ni rahisi pia hata tunapoona barabara imekatika ni rahisi kuwaita na kufika kwenye eneo la tukio na kutengeneza vizuri.”alisisitiza diwani huyo mteule.
Kwa mujibu wa Shagembe daraja la mto Msosa limejengwa kwa kiwango kizuri sana na linaonekana kuwa ni daraja zuri na limejengwa na wakandarasi wazawa ambao ni wananchi wa hapa hapa Tanzania.
“Kwa hiyo tunaendelea kuomba Rais wetu aendelee kuwaamini na kuwapa kipaumbele wazawa waendelee kusimamia miradi yetu inayojengwa kwa fedha za walipakodi wenyewe.”alifafanua zaidi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ighombwe,Iren Bakari alisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kuondokana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili zaidi ya wananchi 19,000 wa kata za Iyumbu,Mgungira pamoja na Ighombwe wanaolitumia daraja hilo.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Dkt John Magufuli kwa kutusaidia kuhusiana na hili daraja, ilikuwa ni adha kubwa kwa sababu mvua ikinyesha haijalishi mvua imenyesha wapi,haijalishi iwe imenyesha Singida mjini au iwe imenyesha huku adha ilikuwa ni kubwa sana kwa mto kujaa.” aliweka bayana.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa Kata mvua zilipokuwa zikinyesha mto ulikuwa ukijaa magari yalikuwa hayapiti na daraja lilikuwa limebomoka na hivyo kukawa na changamoto kidogo kwa sababu daraja hili linatumiwa na zaidi ya watu 19,000 waliopo kata ya Ighombwe na kata za jirani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi ya KAGWA yenye makao yake makuu mjini Singida, Janes Ezra alisisitza kwamba kazi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja inatarajia kukamilika kabla ya wakati uliopo katika mkataba.
“Hii kazi mkataba wetu ni siku 240 lakini mpaka sasa hivi tumefikia asilimia 95 tuna siku 88,au tuseme kama siku 90 kwa hiyo tupo ndani ya wakati maana mkataba wetu unatakiwa uishe aprili,mwakani lakini ndani ya siku saba zijazo tutakuwa tumemaliza kazi yetu na kukabidhi serikali kwa wakati,kwa hiyo tunawatoa wasiwasi wananchi wa maeneo haya na abiria kwamba hii kazi itaisha kwa wakati kabla ya mvua na kipindi cha masika watu watapita salama.”alisisitiza Mkurugenzi Kagwa.
Samweli Moleli ni dereva wa magari makubwa yaliyokuwa yakitumia barabara pamoja na daraja hilo la mto msosa alisisitiza kwamba awali barabara hiyo haikuwa ya kuridhisha sana, isipokuwa hivi sasa wanayafurahia matengenezo ya barabara na daraja hilo yanayokaribia kufikia tamati.
Naye Ayubu Ramadhani mkazi wa Kijiji cha Ighombwe akizungumzia wakandarasi wazawa aliweka wazi kwamba mkandarasi wa kampuni ya Kagwa amelitendea haki sana daraja hilo pamoja na kuwawakilisha kikamilifu wakandarasi wengine wazawa kwa kufanya kazi nzuri na yenye kiwango.
“Kwa upande wa mkandarasi huyu Kagwa tunamshukuru sana kwa sababu amejenga daraja kubwa na lenye kiwango kuliko hata mchina tulikuwa tumezoea madaraja makubwa kama haya yanajengwa na wachina,wanatoka sijui nje ya nchi huko,lakini daraja kubwa lenye kiwango kama hili limejengwa na Kagwa ambaye ni wa humu humu mzawa.”alisisitiza mkazi huyo.
Mradi wa ujenzi wa daraja la mto Msosa linalotumiwa na zaidi ya wananchi 19,000 kutoka kata za Iyumbu,Mgungira pamoja na Ighombwe na kuunganisha mikoa ya Singida na Tabora, litakapokamilika litagharimu zaidi ya shilingi bilioni moja za kitanzania.