WAGONJWA WANNE WA MOYO WAWEKEWA KIFAA CHA KUSADIA MOYO KUFANYA KAZI

Wagonjwa wanne wenye matatizo ya kutanuka kwa moyo, uwezo wa moyo kusukuma damu kuwa chini ya asilimia 50, mfumo wa umeme wa moyo kuwa na shida iliyopelekea moyo kutokufanya kazi sawasawa wamewekewa kifaa cha  kuusadia moyo kufanya kazi vizuri kijulikanacho kitaalamu kwa jina la Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRT-D.

Wagonjwa hao waliwekewa kifaa hicho katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa  kwa muda wa siku mbili na wataalamu wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Ad

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo Yona Gandye alisema wagonjwa waliowekewa vifaa hivyo mfumo wao wa umeme wa moyo ulikuwa na hitilafu kubwa hali iliyopeleka moyo kushindwa kusukuma damu ya kutosha mwilini.

Wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakimwekea kifaa cha  kuusadia moyo kufanya kazi vizuri kijulikanacho kitaalamu kwa jina la Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRT-D mgonjwa ambaye uwezo wa moyo wake  kusukuma damu uko chini ya asilimia 50 wakati wa kambi maalum ya siku mbili iliyofanywa na madaktari wa Taasisi hiyo hivi karibuni.

“Wengi wao walikuwa wanalalamika kuchoka kutwa nzima na hivyo  kushindwa kufanya shughuli zao vizuri na kukosa pumzi. Wagonjwa hawa tumewawekea kifaa  cha High Power Device (CRT- D) ambacho kitausaidia moyo kufanya kazi vizuri hivyo basi wataweza kuendelea na maisha yao kama kawaida”, alisema Dkt. Gandye.

Alizitaja sababu za kutanuka kwa moyo kuwa ni magonjwa hatarishi kama sukari, shinikizo la juu la damu,uzito mkubwa,uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, urithi kutoka kwa wazazi, maambukizi yanayotokana na virusi au bakteria au fungus.

Dkt. Gandye alisema katika kambi hiyo pia walimtibu mgonjwa mmoja aliyekuwa na tatizo la mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida  (zaidi ya mapigo 200 kwa dakika) kawaida huwa ni 60 hadi 90 kwa dakika.

“Kabla ya kumtibu mgonjwa huyu tuliuchunguza moyo ili kubaini chanzo na njia inayosababisha mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida na baada ya kubaini sehemu hiyo tuliithibiti kwa kuziziba au kuziunguza njia hizo kwa jina la kitaalamu matibabu hayo yanajulikana  kama Electrophysiological (EP) studies & ablation”.

“Kimaumbile mtu mwenye tatizo hili moyo wake hauna  shida  lakini una hitilafu kwenye mfumo wa umeme wa moyo hali hii ilipelekea moyo kudunda kwa haraka  zaidi. Dalili za ugonjwa huu ni kusikia mapigo ya moyo yakidunda, kuzimia na pumzi kubana”, alisema Dkt.Gandye.

Alizitaja sababu za moyo kuwa na hitilafu ya mfumo wa umeme ni mtu kuzaliwa na hitilafu hii.

Wakizungumza wakiwa wodini wakiendelea na matibabu wagonjwa waliowekewa vifaa hivyo walisema tangu wamewekewa hali ya mwili kuchoka imepungua sana  pia wanapata pumzi vizuri tofauti na ilivyokuwa awali.

Bibi Safira Chirege kutoka wilayani Ukerewe alisema kabla hajafika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete mwezi wa kwanza mwaka huu kwa ajili ya matibabu alikuwa na tatizo la kifua kubana na hakuwa anaweza kuongea sana na miguu ilikuwa inavimba.

“Kama unavyoniona baada ya kuwekea kifaa hicho sasa hivi naweza kuongea vizuri, ninapata pumzi vizuri na ninaweza kutembea. Hapa nilipo ninamaumivu ya kidonda tu mahali ambapo wameniweka kifaa hiki na ninaamini kikipona nitakuwa mzima kama zamani”, alisema Bibi Sarafina.

Alisema kabla ya kufika JKCI miaka mitatu iliyopita alikuwa anatibiwa katika Hospitali mbalimbali alilazwa Ukerewe na kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua mara moja na pia alitibiwa Morogoro na kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua mara mbili.

Tangu mwaka 2016 jumla ya wagonjwa 31 wameshawekewa vifaa hivyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa upande wa matibabu ya  tatizo la mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida  (Electrophysiological (EP) studies & ablation) wagonjwa watano wameshafanyiwa tiba hiyo ambayo  iliyoanza mwaka 2019.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *