MAFUNDI SIMU ACHENI KUFUTA IMEI NAMBA – WAZIRI NDUGULILE

Na Prisca Ulomi, WMTH, Arusha

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewaasa baadhi ya mafundi simu za mkononi kuacha tabia ya kufuta IMEI namba wanapoletewa simu na wateja wao.

Ad

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya siku ya kwanza mkoani Arusha wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wa mkoani humo alipotembelea taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ya kukagua utendaji kazi wa taasisi hizo baada yakufikisha siku 100 tangu kuundwa kwa Wizara hiyo mpya

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi Imelda Salum kuhusu kifaa kinachotumika kupima masafa ya redio wakati akiwa kwenye ziara yake mkoani Arusha

Amesema kuwa baadhi ya mafundi simu wasio waaminifu wanatumika kufuta IMEI (International Mobile Equipment Identity) namba za simu za mkononi za wateja wao ili simu hizo ziweze kutumika tena ambapo kitendo hicho ni kosa kisheria na Serikali itawachukulia hatua kali mafundi watakaobainika kufanya tabia hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010

Amezungumza hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa TCRA, Mhandisi Imelda Salum kuhusu mafunzo maalumu yaliyotolewa kwa mafundi simu 332 wa Kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara ambapo ameeleza kuwa mafunzo hayo yanayotolewa na Chuo cha VETA na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na kufadhiliwa na TCRA yanawawezesha mafundi simu kujiepusha na vitendo vya uhalifu hususan wizi wa simu na makosa ya mtandaoni; kurasimisha shughuli zao; kuzingatia weledi; kuwawezesha kutoa huduma nzuri kwa wateja na kusaidia Jeshi la Polisi kwenye masuala ya uhalifu hususan wizi wa simu

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Kanda ya Kaskazini (hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani Arusha

Mhandisi Salum ametoa rai kwa wawekezaji wa sekta ndogo ya utangazaji kujenga studio za redio kwenye kanda hiyo kwa kuwa baadhi ya maeneo hayana usikivu wa redio wa kuridhisha na kwa kufanya hivyo kutachochea maendeleo ya wananchi kwa kuwa kanda hiyo ina fursa katika sekta ya utalii na hivyo vifaa na huduma za mawasiliano vinatumika ipasavyo

Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ameielekeza TCRA kuangalia namna ya kupunguza gharama za usajili na utoaji leseni kwa wamiliki wa runinga za mtandaoni (Online TV) kwa kuwa eneo hili linawapatia vijana wengi ajira na gharama za usajili na leseni ni kubwa. Pia, ameielekeza TCRA wapunguze muda walioweka wa kuendelea kusajili wamiliki hao kwa kuwa mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ni mbali

Meneja wa Shirika la Posta Tanzania wa Mkoa wa Arusha, Athman Msilikale akifafanua jambo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake kwenye Shirika hilo mkoani humo. Wa kwanza kushoto anayesikiliza ni Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe

Vile vile, amewataka wafanyakazi wa TTCL mkoa wa Arusha kuwa wabunifu na kuongeza wateja ili kukuza mapato ya Shirika hilo kwa kuwa mkoa huo ni mkoa wa kimkakati na wafanikisheni upatikanaji wa uhakika wa huduma ya intaneti kwa watalii wakiwa maneno ya mbuga za wanayama na waendeshe shughuli za utalii mtandao kwa kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya utalii

Aidha, amelitaka Shirika la Posta Tanzania kutengeneza na kuboresha mifumo ya uendeshaji wa Shirika ili kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inayotoa huduma kwa wateja inasomana kuanzia mteja anapowasilisha barua yake, kifurushi au kupata huduma yoyote mpaka hatua ya kulipia na kuweka kumbu kumbu ya huduma iliyotolewa kwa mteja aliyehudumiwa kwa kutumia njia ya kielektroniki badala ya kufanya huduma hizo kizamani kwa kuandika kwenye karatasi au kila kitengo kufanya kazi peke yake bila ya mifumo iliyopo kusomana na mifumo mingine

Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wa Mkoa wa Arusha wakimsikiliza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati wa ziara yake mkoani humo ya kukagua utendaji kazi wa Shirika hilo

Naye Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa ziara hiyo na kuahidi kuwa watafanikisha maboresho hayo ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhudumia wananchi kwa mtazamo wa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya kufanya kazi kwa Mtazamo Mpya, Utendaji Mpya.

Dkt. Ndugulile anaendelea na ziara yake mkoani Arusha ya kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na taasisi zake pamoja na kuhabarisha umma mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 tangu kuundwa kwa Wizara hiyo mwezi Disemba mwaka jana

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *