Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewaomba wanawake nchini kushikamana ili kuhakikisha wanamchagua mwanamke kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Rais Samia amesema hayo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam iliyokuwa na kaulimbiu “Ajenda ya Mwanamke ni Turufu ya Ushindi”
Amesema kwasasa Rais aliyepo madarakani amewekwa kwa kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba hivyo amewaomba wanawake kuhakikisha kuwa mwaka 2025 wanamuweka madarakani Rais mwanamke.
Rais Samia amewataka wanawake kuhakikisha fadhila walizopewa na Mungu hawaziachii kwa kuwa wanawake wamefanya kazi kubwa ya kuleta uhuru, kujenga siasa na kuwabeba wanaume katika siasa za nchi, hivyo iwapo wataziachia fadhila hizo Mungu atawalaani.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia kama inavyotamkwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1).
Pia amesema Tanzania inaongoza kwa Uhuru wa vyombo vya Habari kwa kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo kati ya hivyo asilimia 75 vinamilikiwa na watu binafsi.
Vilevile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itajitahidi kushughulikia masuala ya haki za wanawake na usawa wa jinsia ili kukuza demokrasia nchini, ikiwemo kutekeleza yaliyomo kwenye Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
Rais Samia amesema Demokrasia inahusiana kwa karibu na masuala ya haki ya kuishi hivyo wananchi wachukue tahadhari dhidi ya UVIKO 19 kwa kupata chanjo kwa hiyari ili kupunguza madhara yatokanayo na janga hilo ikiwa ni pamoja na vifo.
Katika maadhimisho hayo, Mhe. Rais Samia amekabidhiwa Tuzo kama kiashiria cha ushindi wa mwanamke Mtanzania iliyotolewa Azaki ya Tanzania Women Cross – Party Platform/ ULINGO.