WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI

Na Dorina G. Makaya na Ebeneza Mollel Dar-es-salaam.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Yusuf Makamba, amewataka watanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania ili kujiongezea kipato na utaalam kwani sehemu kubwa ya bomba linapita nchini Tanzania.

Ad

Waziri Makamba ameyasema hayo leo tarehe 23 Septemba, 2021 wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa Sekta Binafsi na kampuni zitakazojenga Mradi wa Bomba la Mafuta lililofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Waziri Makamba amesema, mradi huo ni mradi muhimu kwa Tanzania, kwani ni mradi unaosafirisha mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga na kuwa asilimia 80 ya bomba la mafuta litajengwa upande wa Tanzania na hivyo watanzania wanahimizwa kuwa tayari kutumia fursa zitakazotokana na utekelezaji wa Mradi huo.

Waziri wa Nishati Mhe. January  Makamba akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanya ufunguzi wa Kongamano la kujadili fursa na mahitaji ya Mradi kati ya wadau wa Sekta Binafsi na kampuni zitakazojenga Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki ( EACOP) lililofanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa  Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar-es-Salaam tarehe 23 Septemba, 2021. 

“Hii inaonesha ni jinsi gani uchumi wa Tanzania utanufaika na mradi huu” alisema Waziri Makamba.

“Mathalani, inakadiriwa katika kipindi cha ujenzi zitatolewa takribani ajira 10,000 na pia katika kipindi cha uendeshaji zitatolewa takribani ajira 1,000 kwa Watanzania. Hivyo, ni matumaini yangu kuwa washiriki wote ikiwemo Sekta Binafsi itajipanga kikamilifu kutumia fursa hii na kuhakikisha kuwa, yale maeneo ambayo huduma zinaweza kupatikana ndani ya nchi basi fursa hizo zitolewe kwa watanzania.’ Aliongeza Waziri Makamba.

Waziri Makamba amebainisha kuwa, mnamo tarehe 20 Mei, 2021, Serikali ilisaini Mkataba wa Msingi wa Mradi (Host Government Agreement [HGA]) kati yake na Mwekezaji, Kampuni ya EACOP ambapo, kupitia Mkataba huu umeainisha baadhi ya huduma na bidhaa zitakazotolewa na Watanzania pekee ikiwemo huduma za usafirishaji, ulinzi, chakula na vinywaji, huduma za malazi na usambazaji wa mafuta kwa ajili ya magari na mitambo. Amezitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana hapa nchini, shughuli za ujenzi, huduma za mawasiliano na ukodishaji wa mitambo ya ujenzi.

Aidha, Waziri Makamba amebainisha kuwa, bidhaa na huduma nyingine za manunuzi tofauti na zile zilizotengwa kwa Watanzania zitapatikana kwa njia ya ushindani wa kimataifa na Watanzania wenye uwezo, vigezo na sifa stahiki wajitokeze kushiriki.

Amesema, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, inasisitiza ushiriki wa watanzania katika miradi ya nishati inayotekelezwa nchini.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, mradi huu ni wa kimkakati na wa kihistoria utakaotoa fursa nyingi na utagharimu takriban shilingi trilioni 8.

Akizungumzia kuhusu lengo la kongamano, Waziri Makamba amesema, kongamano hilo limelenga kuzikutanisha kampuni zilizoshinda zabuni mbalimbali za ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta na wadau wa sekta binafsi nchini ili waweze kueleza mahitaji yao na utaratibu utakaokuwepo kwa watanzania kuweza kushiriki kutoa huduma mbalimbali wakati wa ujenzi wa mradi. Pia, kuwa na fursa ya majadiliano ya pamoja jinsi ya kufanya maandalizi muhimu ili kufikia matarajio ya wakandarasi wa mradi.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi wa Afrika Mashariki (EACOP) utahusisha ujenzi wa Bomba la Mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima – Uganda hadi Chongoleni Tanga.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, Kati ya kilomita 1,443 zitakazojengwa, kilometa 1,147 ziko upande wa Tanzania na kilometa 296 upande wa Uganda.

Aidha, mradi utahusisha ujenzi wa Kambi 18 ambapo kati ya hizo, kambi 14 ziko upande wa Tanzania na 4 zipo upande Uganda.  Pia, eneo litakalotumika kujenga Coating yard litakuwa wilayani Nzega, Tabora; Vituo 6 vya kusukuma Mafuta ambapo vituo 4 vitajengwa Tanzania na vituo 2 vitajengwa Uganda.

Vile vile. Waziri Makamba amebainisha kuwa, Vituo 2 vya kupunguza kasi ya Mafuta vitajengwa Tanzania na Matanki manne (4) yenye Ujazo wa Mapipa 500,000 kila moja yatajengwa katika eneo la Chongoleani, Tanga pamoja na ghati la kupakia mafuta kwenye meli lenye urefu wa kilometa 1.9.

Akizungumzia kuhusu fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi, Waziri Makamba amesema, hadi sasa, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya EACOP, tayari imelipa Jumla ya shilingi 2,286,540,906 kwa wananchi 351 kama fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa Kambi 14 za mradi na hivyo maeneo yapo tayari kwa kuanza utekelezaji wa mradi.

Amesema, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 259.96 sawa na dola za marekani milioni 112 ikiwa ni mchango wake katika kushiriki kwenye Mradi. Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa, Tarehe 30 Juni, 2021 Serikali kupitia Bunge la Jumhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha Sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa EACOP.

Waziri Makamba ametoa rai kwa Kampuni ya EACOP na washirika wake kuharakisha mchakato wa manunuzi na kuanza rasmi ujenzi wa mradi mwezi Oktoba, 2021 kama ilivyopangwa.

Aidha, ameeleza kuwa, serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuwajengea watanzania uwezo stahiki ili waweze kushiriki kikamilifu katika mradi wa EACOP na miradi mingine ya kimkakati.

Waziri Makamba ameipongeza Serikali, Shirika la Maendeleo ya Mafuta Nchini (TPDC), Kampuni inayoendesha mradi wa bomba (EACOP) na Sekta Binafsi, kwa kuratibu maandalizi ya kongamano hilo na kueleza kuwa, Serikali itaendelea kufanya uelimishaji juu ya fursa za mradi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya na vijiji pamoja na kuandaa makongamano mbalimbali.

Aidha, ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni ya EACOP kuratibu makongamano ya Wadau kwa lengo la kupeana taarifa ya utekelezaji wa mradi na kujadili fursa na mahitaji ya Mradi kwa ujumla ili kuwawezesha watanzania na wadau wote kiujumla kufahamu fursa kwa upana wake na jinsi gani waweze kujiandaa na kushiriki ipasavyo.

Mkutano huo wa wadau wa bomba la mafuta, umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,Mhe. Seif Gulamali,Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,Mha. Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,Kheri Mahimbali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Halfani Halfani,Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio,Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya EACOP,Bw. Matin Tiffen, Wakurugenzi wa Taasisi na Wenyeviti wa Taasisi za Sekta Binafsi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Oni moja

  1. Can you be more specific about the content of your article? After reading it, I still have some doubts. Hope you can help me.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *