WALIOKIUKA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA WAKALIA KUTI KAVU

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba, wakifungua ripoti ya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/21, kushoto ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Prof. Ninatubu Lema, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufazifanyia ukaguzi na uchunguzi wa kina Halmashauri 4 za Wilaya na Taasisi moja ya Serikali kwa kukiuka Sheria za Ununuzi wa Umma.

Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo baada ya kupokea Ripoti ya Tathimni ya Utendaji ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ya Mwaka wa Fedha 2020/2021, jijini Dodoma.

Ad

Dkt. Mwigulu amesema kuwa uchunguzi lazima ufanyike ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watu wote watakaobainika kukiuka taratibu za ununuzi ikiwemo kutoa zabuni nje ya mfumo wa kieletroniki wa TANePS unaotumika kuchakata zabuni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba, ripoti ya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/21, kushoto ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma PPRA, Profesa Ninatubu Lema kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA Prof. Marten Lumbanga, Taasisi tano zilizopata wastani hafifu wa kufuata sheria taratibu na kanuni za ununuzi wa umma kuwa ni Halmashauri ya Mji Kondoa, Halmashauri ya Mbogwe, Halmashauri ya Biharamulo, Halmashauri ya Chato na Taasisi ya Utafiti wa Wanyama.

Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, kuziandikia waraka Taasisi 172 ambazo zimeunganishwa kwenye Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (TANePS) watoe sababu za  kutotumia mfumo huo katika kufanya ununuzi.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa agizo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi na uchunguzi wa kina kwa Taasisi tano zilizofanya vibaya katika shughuli za manunuzi ili kubaini tatizo lililosababisha Taasisi hizo kufanya vibaya kwenye mchakato wa manunuzi baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), jijini Dodoma.

Alizitaka pia Taasisi nunuzi zote kutumia asilimia 30 ya gharama yote ya zabuni zinazotangazwa katika mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya kuyawezesha makundi maalumu yakiwemo ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya ununuzi.

“Nimesikitika sana baada ya kusikia kwamba kati ya Taasisi 86 mlizozikagua ni Taasisi mbili tu ndizo zilitenga asilimia 30 katika mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi maalumu,” alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Mjumbe na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Prof. Ninatubu Lema, alisema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 walifanya ukaguzi wa mikataba 8,838 ya ununuzi yenye thamani ya Sh. trilioni 9.2 kutoka Taasisi 86.

Prof. Lema alifafanua kuwa matokeo ya ukaguzi huo yalionesha kuwa Taasisi 130 kati ya 718 zilizounganishwa kwenye mfumo wa Ununuzi wa TANePS hazikuwasilisha mipango yao ya ununuzi kupitia mfumo huo huku Taasisi 208 ziliwasilisha mipango yao kupitia mfumo huo lakini zikachakata zabuni nje ya mfumo hali inayoashiria kuwepo kwa vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kulia) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Prof. Ninatubu Lema wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine kutoka PPRA na Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/21, jijini Dodoma.

Na: Josephine Majura na Alice Nyange WFM – DODOMA

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alimhakikishia Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atafuatilia maelekezo aliyopewa na kuwawajibisha wale wote watakaobainika kuhusika na ukiukaji wa Sheria ya ununuzi na pia kuangalia uwezo wao wa utendaji kazi na namna ya kuwajengea uwezo.

Alisema kuwa ni muhimu taasisi za umma zikazingatia sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa umma ili kuthaminisha miradi ya maendeleo na fedha zinazotumika kwani sekta ya ununuzi inatumia kiasi kikubwa cha Bajeti ya Serikali ambapo kwa mwaka 2020/2021, bajeti ya ununuzi ilikuwa shilingi trilioni 25 sawa na zaidi ya asilimia 75 ya Bajeti yote ya Serikali.

Bw. Tutuba alisema kuwa Mfumo wa ununuzi wa TANePS unaleta uwazi na uwajibikaji katika ununuzi ili fedha za umma zinazotolewa na Serikali ziweze kuleta manufaa kwa wananchi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *