- Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati na kuongeza kina cha kupakia na kupakua mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam
- Nditiye amesema kuwa ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya maendeleo ya mradi huo kwa kufikia kiwango cha asilimia 42 ya mradi huo ambapo mradi huo ulitegemewa ukabidhiwe mwezi Oktoba mwaka huu 2018. Amefafanua kuwa ilibidi mradi huo ufanyiwe maboresho ili kuendana na matakwa ya mradi ili uweze kubeba mizigo mizito na utakamilika mwezi Juni mwakani, 2019.
- Pia, ameongeza kuwa, ili kuweza kwenda sambasamba na muda wa mkataba wa mradi huo, ujenzi wa gati namba moja ulikuwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu, 2018 badala ya mwezi Aprili mwakani 2019, “hivyo tuko ndani ya muda wa mkataba,” amesema Nditiye.
- Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Karim Mataka amemweleza Nditiye kuwa maendeleo ya mradi ni mazuri japo walikumbana na changamoto ya kukukutana na udongo laini baharini kwenye eneo la ujenzi wa mradi huo ambapo iliwalazimu kuimarisha eneo hilo ili bandari iweze kubeba mzigo wa kontena mpaka tano zikiwa zimepandana kutokea chini kwenye eneo la kupakia na kupakua mizigo
- Mataka ameongeza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imejipanga ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ndani ya kipindi cha miezi 36 kuendana na matakwa ya mkataba wa mradi huo ambao ulianza rasmi tarehe moja Julai mwaka 2017 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020. Mataka amesema kuwa mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 336 na unajengwa na mkandarasi wa kampuni ya kutoka China ya CHEC (LYU wei)
- Amefafanua kuwa mradi wa upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati na kuongeza kina cha kupakia na kupakua mizigo, utaiwezesha bandari kuhudumia meli kubwa zaidi ambapo hivi sasa hamna kina cha mita 12 ambapo inazifanya meli nyingi kuwa kwenye foleni na kulazimika kusogeza meli moja moja ambapo mradi huu ukikamilika, bandari itakuwa na uwezo wa kushusha mizigo ya kutoka kweye meli kubwa saba kwa wakati mmoja
Ad