Mjumbe wa bodi Dkt. Grace Magembe akichangia jambo katika kikao hicho kilichofanyika katika Hospitali ya Mloganzila.

MLOGANZILA IMEBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI NA ITAENDELEA KUBORESHA ZAIDI – PROF.MAJINGE

  • Bodi ya Wadhamini, Hospitali ya Taifa Muhimbili imeupongeza Uongozi wa kwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika Hospitali ya Mloganzila.
  • Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Prof. Charles Majinge katika kikao cha kawaida cha Bodi hiyo kilichofanyika Hospitali ya Mloganzila ambapo Menejimenti iliwasilisha taarifa ya utendaji kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka cha Oktoba hadi Desemba, 2018.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Charles Majinge (kulia) akizungumza katika kikao cha kawaida cha bodi hiyo kilichofanyika katika Hospitali ya Mloganzila ambapo Menejimenti iliwasilisha taarifa ya utendaji kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, Oktoba hadi Desemba, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru.
  • “Napenda kwa dhati kabisa mfahamu kuwatunaridhishwa sana na utendaji kazi wa Hospitali ya Mloganzila kwani hata malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi kuhusu utoaji wa huduma yanaendelea kupungua siku hadi siku, hivyo hii ni hatua nzuri na ya kupongezwa”, alisema Prof. Majinge.
  • Sisi kama Bodi ya Wadhamini, tunaomba kila mmoja wenu atimize wajibu wake mahali pake pa kazi ili Mloganzila iwe moja ya hospitali bora hapa nchini katika kutoa huduma za kibingwa, kufundisha na kufanya tafiti, alisisitiza Prof. Majinge.
WAJUMBE
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Wakurugenzi wa Hospitali hiyo wakimsikiliza Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Charles Majinge alipokua akizungumza katika kikao hicho.
  • Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ambaye pia ndiye mwenye dhamana ya kusimamia Hospitali ya Mloganzila alisema pamoja na hospitali hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali, Menejimenti imejipanga kuhakikisha inatoa huduma za kibingwa na za kibobezi kama ilivyokusudiwa.
  • Naye Kaimu, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka ambapo wagonjwa wa nje 20,173 walihudumiwa ukilinganisha na wagonjwa 17,116 waliohudumiwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 17.8.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (wapili kushoto) akiwaelezea wajumbe wa bodi utoaji wa huduma katika hospitali hiyo. Wajumbe hao wamepata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma katika hospitali hiyo.
  • Dkt. Magandi amesema upande wa wagonjwa waliolazwa kulikuwa na ongezeko la asilimia 29.6 kutoka wagonjwa 1,459 hadi 1,891, wakati upande wa huduma za upasuaji jumla ya wagonjwa 649 walifanyiwa upasuaji  ukilinganisha na upasuaji wa wagonjwa 267 katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha ambalo ni ongezeko la  asilimia 143.
  • Kwa upande wa huduma za tiba shirikishi inayojumuisha maabara na huduma za radiolojia kulikuwa na ongezeko la huduma ambapo maabara ilipokea jumla ya sampuli za vipimo mbalimbali 28,907 kwa wagonjwa waliolazwa na wa nje ukilinganisha na sampuli 16,233 katika robo ya kwanza ya mwaka ikionesha ongezeko la sampuli 12,674 ni sawa na asilimia 78, alisema Dkt. Magandi.
MJUMBE WA BODI
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Andrea Pembe (kushoto) akizungumza katika kikao hicho, kulia ni Meya wa Jiji la Dar es salaam Mh. Isaya Mwita ambaye ni mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo.
  • Dkt. Magandi alisema katika huduma za radiolojia zinazojumuisha vipimo vya CT scan, MRI, X-ray n.k kulikuwa na ongezeko la vipimo asilimia 47 ambapo vipimo 5,221 vilipimwa katika kipindi hicho ukilinganisha na vipimo 3,541 na huduma katika maeneo yote ya Hospitali zinaendelea kuimarishwa siku hadi siku.
  • Oktoba 3, 2018 Serikali iliiweka Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MAMC) Mloganzila chini ya Mamlaka ya Usimamizi na Uendeshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *