- Jumla ya wagonjwa 12 wamefanyiwa uchunguzi wa kuangalia jinsi mishipa ya damu ya moyo inavyofanya kazi kupitia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara ya uchunguzi na tiba ya mishipa ya damu ya moyo.
- Uchunguzi huo ambao umefanyika kwa siku mbili umefanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma.
- Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema kati ya wagonjwa 12 waliofanyiwa uchunguzi watano wamekutwa na matatizo ya mishipa ya damu kutopitisha damu vizuri, wanne wanahitaji matibabu ya kuzibuliwa mishipa ya damu na mmoja atatumia dawa.
- “Tumefanya uchunguzi kwa wagonjwa 12 , tisa wanamatatizo madogo ambayo hayahitaji matibabu makubwa na wanne wanahitaji matibabu makubwa ambayo ni kuzibuliwa kwa mishipa ya damu na mmoja atatumia dawa”, alisema Prof. Janabi .
- Kwa upande wa wagonjwa waliofanyiwa uchunguzi waliishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hiyo katika mkoa wa Dodoma ambapo wagonjwa wenye matatizo kama hayo wataweza kupata huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamini Mkapa badala ya kusafiri kwenda mkoani Dar es Salaam kufuata huduma hiyo.
- Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwalimu Mstaafu Simon Mesomapya ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mtanana wilayani Kongwa alisema alianza kusumbuliwa na maradhi ya moyo mwaka 2016 na kutibiwa katika Hospitali mbalimbali ambapo mwaka huu alipewa rufaa ya kutibiwa BMH kwa uchunguzi zaidi.
- “Kupatikana kwa huduma hii hapa BMH itapunguza gharama za kusafiri kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi pia Dodoma ni kati kati ya nchi ni rahisi kwa wananchi wa mikoa jirani kupata huduma hiyo”, alisema Mwalimu Mesomapya.
- Aliiomba Serikali iendelee kuboresha huduma hiyo ili wananchi wenye matatizo ya moyo waweze kufurahia huduma hiyo,
- Mtambo huo wa kisasa wa Cathlab ambao ni maabara ya uchunguzi na matibabu ya mishipa ya moyo unauwezo pia wa kuchunguza mishipa ya damu ya mikono, miguu na kichwa.
Ad