SERIKALI KUPAMBANA KUMKOMBOA MWANANCHI MNYONGE – DKT. MAHIGA

  • Serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake ili kumkomboa mwananchi mnyonge ili kila mtu apate haki na kuwa sawa na mwingine na ashiriki kujenga uchumi wa viwanda.
  • Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema hayo alipokuwa akizungumza na wasajili wasaidizi wa watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini katika kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria linalofanyika jijini Arusha.
WASHIRIKI
washiriki wa kongamano wakisikiliza maelezo mbalimbali kutoka kwa viongozi waliokuwa wakizungumza nao wakati wa kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria lililofanyika jijini Arusha
  • “Tumetunga Sheria ya Msaada wa Kisheria na tunaitekeleza kwa dhati, niwahakikishie kuwa tunafanya kila lililo ndani ya uwezo wa Serikali kumkomboa mwanchi mnyonge ili kila mmoja ajione ana haki sawa na mwenzake na aweze kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda ambayo ndio dira ya Serikali,” alisema Dkt. Mahiga.
  • Amesema Serikali inatamani kuona upatikanaji haki na msaada wa kisheria unaongezeka na kuwafikia wananchi kule waliko na kuongeza kuwa wasajili wasaidizi wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha watoa huduma ya msaada wa kisheria katika maeneo yao wanawafikia wananchi wengi zaidi huku wakitoa huduma bora.
NAIBU KATIBU MKUU
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju akitoa neno wakati wa kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini lililofanyika jijini Arusha.
  • Waziri Mahiga amewataka wasajili wasaidizi hao kutoka katika Halmashauri za Wilaya zote nchini, miji na majiji kuweka mikakati ya namna bora ya kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao ili kufikia lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wengi na  kwa kiwango kilicho bora.
  • Amesema Serikali kupitia Sheria ya Msaada wa Kisheria No.1 ya Mwaka 2017 itaendelea kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa haki kwa wakati huku misingi ya utawala bora unaozingatia wajibu, sheria na demokrasia.
KATIBU MKUU
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akizungumza na wasajili wasaidizi wakati wa kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini linalofanyika jijini Arusha.
  • Awali akizungumza katika Kongamano hilo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome aliwakumbusha wasajili wasaidizi hao kuwa wasimamizi wazuri wa watoa huduma kwakuwa wao ni kiungo kati ya Serikali na watoa huduma hao.
  • Aliwataka kuzingatia kuwa huduma  ya msaada wa kisheria ni kazi ya kujitolea yenye kuhitaji uadilifu wa hali ya juu huku akiongeza kuwa kazi hiyo ni sawa na utoaji wa huduma za kiroho ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa dini mbalimbali nchini.
MSAJILI
Msajili wa watoa huduma ya msaada wa Kisheria nchini Kutoka Wizara y aKatiba na Sheria Bibi Felista Mushi akizungumza wakati wa kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wenye uhitaji nchini linalofanyika jijini Arusha
  • Kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini limewezesha wasajili wasaidizi ambao ni maafisa maendeleo ya jamii nchini kukaa pamoja na wizara ya Katiba na Sheria yenye dhamana ya kuratibu utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini na kujadiliana juu ya namna ya kuendesha gurudumu la msaada wa kisheria na kuangalia changamoto mbalimbali zinazowakabili watoa huduma hizo nchini na kuona jinsi ya kukabiliana nazo.
  • Kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia mradi wa Upatikanaji Haki unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa –UNDP.
Ad

Unaweza kuangalia pia

SPIKA WA BUNGE AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA WILAYA YA KONDOA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb) leo azindua …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *