MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI KATIKA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI WAZINDULIWA

SB
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kulia), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri (wa pili kushoto) na Mratibu wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki, Salum Mnuna (wa kwanza kushoto), wakizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika mradi wa bomba la Mafuta katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega.
  • Serikali imezindua Mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji, Wilaya na Mikoa itakayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ikiwa ni hatua nyingine katika utekelezaji wa mradi huo.
  • Mpango huo umezinduliwa katika Kijiji cha Sojo, Kata ya Igusule, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora tarehe 25/5/2019 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyeambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry na Meneja Mradi wa EACOP, Mantin Tiffen.
SB
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) na Meneja Mradi wa EACOP, Mantin Tiffen wakizungumza mara baada ya kumaliza uzinduzi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika mradi wa bomba la Mafuta katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega.
  • Akizungumza na wananchi wa Sojo, Waziri Lukuvi, alisema kuwa, mpango huo wa matumizi ya ardhi unahusisha Mikoa Nane, Wilaya 24 na Vijiji 226 ambapo vijiji 30 vipo katika Mkoa wa Tabora.
  •  ” Mpango huu unazinduliwa katika Kijiji cha Sojo kwa niaba ya Vijiji vyote nchini kwa kuwa hapa Sojo ndipo patakuwa na kituo kikubwa cha kutoa huduma katika mradi wa  bomba la Mafuta kuliko vituo vingine kwani kutakuwa na  Kambi Kuu na kiwanda cha kutayarisha mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta kitajengwa hapa.” alisema Lukuvi.
  • Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi, alitoa onyo kwa wavamizi wa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya mradi huo kuwa, tayari mkuza wote ulishapigwa picha za anga hivyo  fidia itatolewa kwa wananchi wanaostahili tu.
SB
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, wakifuatilia uzinduzi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika mradi wa bomba la Mafuta katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega.
  • Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema kuwa, kazi za mradi wa EACOP zilizopangwa kufanyika katika Kijiji hicho cha Sojo zina uwekezaji wa shilingi bilioni 600 na matarajio ni kuwa kazi hizo zitaanza mwezi wa Tisa mwaka huu.
  • Alisema kuwa, kutakuwa na ajira zitakazozalishwa hivyo alitoa wito kwa wananchi  kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwekezaji huo.
  • Aliongeza  kuwa, mpaka sasa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi umeshatoa ajira zaidi ya 200 na matarajio ni kuwa utaendelea kutoa ajira zaidi kwa watanzania.
  • Kuhusu umeme, alieleza kuwa, Wizara iko katika Mpango wa kusambaza umeme kwenye Vijiji vyote vinavyopitiwa na mkuza huo kwa gharama ya shilingi elfu 27,000 tu ili kuweka mazingira wezeshi ya kutekeleza mradi husika.
SB
Meneja Mradi wa EACOP, Mantin Tiffen akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika mradi wa bomba la Mafuta katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega.
  • Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alisema kuwa, Mkoa huo utaweka mazingira wezeshi ili mradi huo wa Bomba ufanyike kwa ufanisi na ameahidi kusimamia matumizi bora ya ardhi iliyotengwa kwa ajili ya mradi husika.
  • Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Tanzania, Salum Mnuna, alisema kuwa, Rais John Pombe Magufuli amefanya jitihada mbalimbali zilizowezesha mradi huo kuanza kutekelezwa nchini hivyo ni muhimu kwa wanachi wakafanya bidii kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi.
  • Aliongeza kuwa, mradi huo licha ya kutoa ajira za ujuzi wa juu, kati, chini na vibarua, utaboresha pia baadhi ya miundombinu kama vile Reli na Barabara pamoja na huduma za kijamii katika maeneo ambayo mradi utapita.Na Teresia Mhagama, Tabora
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI KALEMANI AFUNGUA KIWANDA CHA NGUZO ZA UMEME – KIGOMA

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya, kilichopo katika Mtaa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *