WAZIRI KALEMANI ABAINISHA MKAKATI WA KUNUSURU UKOSEFU WA UMEME ULIOTOKEA KAGERA

  • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema serikali inatekeleza miradi kadhaa inayolenga kuunganisha umeme wa gridi ya taifa kwa baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kagera ambazo kwa sasa zinapata huduma ya umeme kutoka Uganda, ili kuzinusuru na adha iliyojitokeza hivi karibuni ya ukosefu wa umeme kwa takribani siku tatu.
  • Aliyasema hayo Agosti 22, 2019 wakati akijibu hoja za baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini katika kikao kilichohusisha uwasilishaji wa taarifa ya uendelezaji wa miradi ya nishati jadidifu nchini.
KL -01
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyo chini ya sekta anayoisimamia mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma, hivi karibuni.
  • Akifafanua, Dkt Kalemani alieleza kuwa changamoto iliyojitokeza Kagera ilitokana na hitilafu katika gridi ya taifa ya Uganda, ambayo iliathiri wilaya za Karagwe, Bukoba Vijijini na sehemu ya Muleba ambazo zinapata huduma husika kutoka nchi hiyo jirani.
  • Alitaja mradi wa kwanza ni unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita, ambao unatarajiwa kukamilika Mei mwakani. “Umeme huo sasa utafika mpaka Karagwe na Bukoba ili kuondoa utegemezi wa umeme kutoka Uganda.”
KL 2-01
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akiongoza kikao cha majumuisho kilichohusisha wataalamu wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake (hawapo pichani), mara baada ya kushiriki kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma, Agosti 22, 2019. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Haji Janabi.
  • Aidha, alitaja mradi mwingine kuwa ni wa Rusumo unaohusisha ujenzi wa njia ya umeme hadi Karagwe ambao unatarajiwa kukamilika Februari, 2020.
  • “Kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha maeneo yote ya Kagera kupata umeme wa gridi ya taifa. Hii ni kwa sababu wilaya za Ngara, Muleba na Biharamulo tayari zinapata umeme huo na ndiyo maana hazikuathirika na changamoto iliyojitokeza hivi karibuni,” alisema.
KL 4-01
Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake, wakiwa katika kikao cha majumuisho mara baada ya kushiriki kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma, Agosti 22, 2019.
  • Awali, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, aliieleza Kamati hiyo kuwa, kupitia sera ya taifa ya nishati ya mwaka 2015, ambayo imeainisha Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta Ndogo ya Umeme, serikali imekuwa ikitilia mkazo uzalishaji wa nishati kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo nishati jadidifu.
  • Alisema, serikali imekuwa ikitekeleza mipango ya kimataifa katika kuendeleza sekta hii ndogo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme, kulinda afya za watu pamoja na kutunza mazingira.
KL 5-01
Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake, wakiwa katika kikao cha majumuisho mara baada ya kushiriki kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma, Agosti 22, 2019.
  • Akizungumzia vyanzo vya nishati jadidifu ambavyo Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imevifanyia utafiti na kuviainisha, Mhandisi Luoga alivitaja kuwa ni pamoja na umeme jua ambao unaweza kuzalisha hadi megawati 1,000 za umeme nchini.
  • Nyingine ni upepo ambao pia unaweza kuzalisha megawati 1,000, jotoardhi (megawati 5,000), tungamotaka ambayo zaidi ni katika matumizi ya kupikia yaani mkaa, kuni pamoja na mabaki ya mimea na mazao, na maporomoko madogo ya maji ambayo kwa mujibu wa tafiti yanaweza kuzalisha hadi megawati 480 za umeme hapa nchini.
  • Katika kikao cha majumuisho na wataalamu, baada ya kukutana na Kamati ya Bunge, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara kuhakikisha wanatekeleza maagizo yaliyotolewa na Kamati, hususan suala la utoaji elimu kwa wazalishaji wadogo wa umeme ili wawe na uelewa namna gani wanapaswa kuzalisha kwa tija.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *