GESI TULIYONAYO LAZIMA ITUMIKE KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA – DKT KALEMANI

 • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema mpango wa serikali wa miaka 30 wa matumizi sahihi ya rasilimali za gesi na mafuta, pamoja na mambo mengine, umelenga kuhakikisha gesi inatumika kujenga uchumi wa viwanda.
 • Akizungumza katika ufunguzi wa Jukwaa la Tisa la Uziduaji, Novemba 6, mwaka huu jijini Dodoma, Dkt Kalemani alisema kiasi cha gesi futi za ujazo trilioni 57.54 ambazo zimeshagunduliwa hadi sasa nchini, zimepangiwa matumizi mbalimbali yanayolenga kufanikisha azma hiyo.
1-01
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akielezea mafanikio ya sekta ya nishati, wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Tisa la Uziduaji, lililofanyika Novemba 6, 2019 jijini Dodoma.
 • Akitoa takwimu, alibainisha kuwa, gesi futi za ujazo trilioni 5.64 zimetengwa kwa ajili ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya mbolea na ‘petrochemicals’ pamoja na kuunganishia wananchi majumbani kwa matumizi ya kupikia.
 • “Kazi hizo zimeanza ambapo tayari mabomba manne ya gesi yamejengwa Dar es Salaam na hadi sasa zaidi ya wananchi 500 wameshaunganishwa,” alieleza.
 • Aidha, alisema kuwa gesi futi za ujazo trilioni 1.1 ni kwa ajili ya kuunganisha katika magari ambapo alibainisha kuwa zaidi ya magari 320 nchini, yameshaunganishwa na zoezi linaendelea.
3-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Wabunge walioshiriki Jukwaa la Tisa la Uziduaji, Novemba 6, 2019 jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
 • Kuhusu matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme, Waziri alieleza kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya gesi inayotumika nchini hivi sasa ni katika kuzalisha umeme. “Zaidi ya asilimia 56 ya umeme tunaopata unatokana na rasilimali ya gesi.”
 • Akifafanua zaidi, alisema sekta ya gesi inaendelea kukua hapa nchini ambapo mahitaji kwa sasa yamefikia kiasi cha futi za ujazo milioni 190 kutoka milioni 175 ya mwaka 2015.
 • Alisema, watanzania wana haki ya kujivunia kukua kwa sekta husika kwani gesi ilipovumbuliwa kwa mara ya kwanza nchini, mwaka 1972 hadi 1082 huko SongoSongo na Mnazi Bay, ilikuwa futi za ujazo mbili tu na sasa imefikia futi za ujazo trilioni 57.54.
4-01
Sehemu ya umati wa washiriki wa Jukwaa la Tisa la Uziduaji wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo, Novemba 6, 2019 jijini Dodoma.
 • Katika hatua nyingine, Waziri alizungumzia suala la ushirikishwaji wazawa katika sekta husika ambapo alieleza kuwa Sheria ya Mwaka 2015 imeweka ukomo wa watanzania kushirikishwa kwa asilimia zisizopungua 25 katika uwekezaji, usimamizi na biashara ya mafuta na gesi nchini.
 • “Hata hivyo, sharia pekee haitoshi, ndiyo maana serikali ikaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha utekelezaji wake ikiwemo kuunda timu ya uratibu, serikali yenyewe kufuatilia ili kujiridhisha na pia kuna kanzidata maalumu kwa ajili ya kuwatambua wawekezaji wazawa katika sekta husika.”
5-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Taasisi za kiraia walioshiriki Jukwaa la Tisa la Uziduaji, Novemba 6, 2019 jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
 • Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa washiriki wa Jukwaa hilo, kuhusu fidia kwa waliopisha mradi wa kuchakata gesi eneo la Likong’o, Kilwa Masoko; Waziri alisema kiasi cha shilingi bilioni 56 za Tanzania zimetengwa na kwamba zoezi la uhakiki likikamilika, wote wanaostahili watalipwa.
 • Jukwaa hilo lilifanyika chini ya uratibu wa Taasisi ya kiraia ya Haki Rasilimali na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya uziduaji wakiwemo viongozi wa serikali, wabunge na wajasiriamali.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *