RAIS MAGUFULI AHUTUBIA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NORDIC NA AFRIKA

  • Rais Dkt. John Magufuli amezishukuru nchi za Nordic kwa uhusiano na ushirikiano wake mzuri na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania na ametoa wito kwa nchi hizo kujielekeza zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi.
  • Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 08 Novemba, 2019 alipohutubia Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
rai 7
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania katika mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre(JNICC)
  • Akizungumza katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na Mawaziri 29 wa nchi za Afrika na Mawaziri 5 wa nchi za Nordic ambazo ni Norway, Sweden, Denmark, Finland na Iceland, Mhe. Rais Magufuli amesema Afrika inakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na nchi za Nordic kabla na baada ya harakati za ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, ambapo zilichangia huduma za kijamii na kiuchumi kama vile afya, elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, nishati, mazingira pamoja na kulinda amani na usalama.
  • Ametolea mfano wa Tanzania ambapo nchi za Nordic zimechangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Kibaha, Chuo cha Utafiti wa Kilimo Uyole, vyuo mbalimbali vya ufundi na kampeni za kufuta ujinga katika miaka ya 70.
rai 1-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Ine Marie Eriksen Soreide mara baada ya kufungua mkutano wa 18 wa Mawaziri wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)
  • Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amesema kuna haja ya kubadilisha mwelekeo na kuingia katika mwelekeo wa kisiasa unaojikita katika ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.
  • Amesisitiza kuwa kwa kuwa nchi za Nordic zenye watu wapatao Milioni 27 zina uchumi mkubwa unaofikia pato la mwaka la Dola za Marekani Trilioni 1.7 ikilinganishwa na nchi za Afrika zenye watu Bilioni 1.2 na pato la mwaka la Dola za Marekani Trilioni 2.334, Afrika inapaswa kujifunza kutoka Nordic na amezikaribisha nchi za Nordic kuja kuwekeza Afrika katika viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao, kuzalisha ajira na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo.
rai 2-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Pekka Haavisto kabla ya kuanza mazungumzo yao katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC).
  • Amebainisha kuwa Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo eneo la ukubwa asilimia 30 ya eneo lote duniani linalofaa kwa kilimo, ukanda wa pwani ya bahari wenye urefu wa kilometa 30,500, mifugo, misitu, wanyamapori, mafuta, gesi, utalii na uchumi wake unaokua vizuri kwa wastani wa asilimia 4.1.
  • Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za Afrika kujenga mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji kutoka nchi za Nordic na amesema kwa kutambua hilo Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuvutia uwekezaji huo zikiwemo kuwa na sheria za kuwalinda wawekezaji, kutekeleza mkakati wa kurekebisha na kuboresha mazingira ya biashara (The Blue Print) na kutenga kanda maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uwekezaji.
rai 3-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Sweden Dkt. Wilbroad Slaa mara baada ya kufungua mkutano wa 18 wa Mawaziri wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)
  • Hatua zingine ni kujenga na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, kujenga meli, kununua ndege pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme.
  • Baada ya kuhutubia mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mhe. Ann Linde, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Marie Eriksen Søreide na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto.
rai 5-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Ann Linde mara baada ya kumkabidhi zawadi ya Kamusi ya Kiswahili na Kingereza pamoja na kitabu cha Kiswahili mara baada ya kufungua mkutano wa Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)
  • Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mawaziri hao kupeleka salamu zake kwa Wakuu wa Nchi zao na amewahakikishia kuwa Tanzania ipo tayari wakati wote kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano uliopo, mkazo zaidi ukiwa katika biashara na uwekezaji.
rai 6-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya kinyago cha mpingo Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Ine Marie Eriksen Soreide kabla ya kuanza mazungumzo yao katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)
  • Mawaziri hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga uchumi kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kupiga vita rushwa na pia wamemuahidi kuendelea kushawishi kampuni za nchi zao kuja kuwekeza Tanzania ikiwemo kampuni kubwa ya Equinor ya Norway ambayo inakamilisha maandalizi ya kuwekeza nchini Tanzania kiwanda cha kusindika gesi (LNG) kitakachogharimu Dola za Marekani Bilioni 20 (sawa na shilingi Trilioni 45.555).
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *