SERIKALI MKOANI SHINYANGA YAKUSANYA  BILIOINI 1.5 KAMA KODI YA MRABAHA NA ADA YA UKAGUZI KUTOKA KWA WACHIMBAJI

  • Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joseph kumburu amesema kuwa utaratibu mzuri uliowekwa kwenye usimamizi wa uzalishaji na biashara ya madini kwa wachimbaji wasio rasmi mkoani Shinyanga umepelekea Serikali kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.56 kama kodi ya mrabaha na ada ya ukaguzi kuanzia mwezi Mei, 2019 hadi Januari, 2020.
  • Mhandisi Kumburu ameyasema hayo tarehe 05 Februari, 2020 kwenye ziara ya maafisa habari kutoka Idara ya Habari MAELEZO na Tume ya Madini yenye lengo la kutengeneza vipindi maalum vyenye kuelezea mafanikio ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini katika mkoa wa Shinyanga tangu kuanzishwa kwake.
  • Alisema kuwa mapema Mei, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alielekeza Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kuhakikisha inaweka utaratibu maalum wa kurasimisha maeneo ya Mwakitolyo yaliyopo mkoani Shinyanga kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake na kulipa kodi mbalimbali Serikalini.

M1-01

  • Aliendelea kusema kuwa, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga ilihamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi vidogo ambapo jumla ya vikundi 23 viliundwa na kupewa leseni za uchimbaji mdogo wa madini.
  • Alisema kuwa, kabla ya kuundwa kwa vikundi na kupewa leseni kwenye eneo hilo, Serikali ilikuwa haijawahi kupata kodi kutoka kwa wachimbaji wadogo wanaotumia mialo kwenye uzalishaji wa madini kwenye eneo hilo kwa sababu madini hayo yalikuwa yanatoroshwa.
  • Katika kuhakikisha Ofisi yake inatatua changamoto hizo, Mhandisi Kumburu alieleza kuwa uliwekwa utaratibu maalum wa kuwasajili wachimbaji wadogo wanaomiliki mialo na kupewa fomu maalum za ukusanyaji wa kodi kabla ya madini hayo kupelekwa kwenye masoko ya madini.
  • Alisema kuwa, fomu husika zililenga kuhakikisha kuwa usimamizi wa biashara ya madini unaanzia kwa mchimbaji kwenda kwa mmiliki wa mwalo ambaye hujaza fomu husika ili kupeleka madini sokoni.
M3-01
Mchimbaji akiendelea na kazi
  • Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini katika Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Kumburu alisema kabla ya kuanzishwa kwake, uzalishaji wa madini ya dhahabu ulikuwa ni kilo 231 kwa thamani ya shilingi bilioni 19.5 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kililipwa kama mrabaha na ada ya ukaguzi na kuongeza kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa masoko ya madini mapema Mei 2019, madini yenye uzito wa kilo 329 yenye thamani ya shilingi bilioni 31.9 yaliuzwa na kiasi cha shilingi bilioni 2.2 kulipwa Serikalini kama mrabaha na ada ya ukaguzi.
  • Aliongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana mara baada ya uanzishwaji wa masoko ya madini kuwa ni pamoja na udhibiti wa utoroshwaji wa madini hali iliyopelekea uzalishaji wa madini katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama kuongezeka kutoka kilo 100 kwa mwaka hadi kilo 1572 tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini na kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9.7 kama mrabaha na ada ya ukaguzi.
  • “Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanza kwa masoko ya madini katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama tulikuwa tunakusanya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 593.6 kwa mwaka, lakini baada ya masoko kuanzishwa hadi kufikia Januari, 2020 tumeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9.7 haya ni mafanikio makubwa,” alisema Mhandisi Kumburu.
  • Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini la Kahama na Kituo cha Ununuzi wa Madini cha Kakola mbali na kupongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye uboreshaji wa Sheria ya Madini na kanuni zake walieleza kuwa, Sekta ya Madini imekuwa na manufaa makubwa sana kwao ikiwa ni pamoja na ongezeko la ajira.
  • Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini la Kahama, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Emmanuel Kidenya alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo kulikuwepo na vikwazo mbalimbali kwenye biashara ya madini ikiwa ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika na kutokuwepo kwa bei elekezi.
  • Alisema kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa soko husika, biashara ya madini imekuwa ni ya uhakika ambapo huuzwa kwa kufuata bei elekezi inayotolewa kila siku kulingana na soko la dunia na kupata faida kubwa.
  • Aliongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na usalama kwenye biashara ya madini, ongezeko la ajira na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika mji wa Kahama.
  • Naye mnunuzi wa madini katika soko hilo, Kayo Ngarama aliongeza kuwa uanzishwaji wa soko husika umeongeza uwazi kwenye biashara ya madini hivyo wafanyabiashara wa madini na Serikali kwa ujumla kunufaika.
  • Naye Kaimu Mwenyekiti wa madalali wa madini katika Kituo cha Ununuzi wa Madini cha Kakola, Baraka Shabani aliongeza kuwa uwepo wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini katika Wilaya ya Kahama umepunguza kwa kiasi kikubwa utoroshwaji wa madini.NA ANDREW CHALE
Ad

Unaweza kuangalia pia

SERIKALI YAJIZATITI KUIMARISHA USIMAMIZI NA UDHIBITI WA RASILIMALI MADINI

Serikali imedhamiria kuwa na mikakati endelevu ya kusimamia na kudhibiti rasilimali madini ili ilete tija …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *