Serikali imesema itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kadri nafasi zitakavyokuwa zikipatikana ili kuboresha huduma za afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Waguzi Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi; Sauti inayoongoza Uuguzi kwa Dunia yenye Afya.”
Waziri Ummy Mwalimu amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kwa sababu kuna uhaba wa wauguzi kwenye vituo vya afya licha ya kuwapo zaidi ya wauguzi 30,451 katika vituo vya umma na binafsi nchini.
Amesema asilimia 80 ya huduma za afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi hivyo Serikali itaendelea kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na wauguzi nchini.
“Wauguzi wamekuwa wapambanaji wakubwa katika kutoa huduma kwa washukiwa wa ugonjwa wa Corona (Covid-19), hivyo hongereni wauguzi wote nchini Tanzania,” amesema Waziri.
Amesema katika jitihada za Serikali za kuboresha huduma za wauguzi na wakunga, Serikali imekamilisha muongozo wa kutoa huduma kwa kuzingatia utu, heshima na maadili.
Waziri wa Afya amesema jumla ya waguzi 778 katika hospitali 15 za rufaa za mkoa wamepatiwa mafunzo muhimu ili kuwezesha mpango wa kutoa huduma rafiki kwa wananchi na kwa kujali utu wao.
“Mafunzo haya yataendelea kutolewa katika ngazi zote za kutoa huduma na tayari tumetengeneza mfumo wa kupokea taarifa za malalamiko na kero kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.