WAZIRI BITEKO: MAKUSANYO SEKTA MADINI YAONGEZEKA KUTOKA BILIONI 39/- HADI BILIONI 58/- KWA MWEZI APRILI

Nuru Mwasampeta na Tito Mselem, Dodoma

Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema ukuaji wa Sekta ya Madini unakua kwa kasi na kuifanya kuwa sekta ya kwanza kwa ukuaji kwa mwaka 2019 ikifuatiwa na sekta ya ujenzi.

Ad

Ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka na kufikia asilimia 17.7 kutoka ukuaji wa asilimia 1.5 kwa mwaka 2018 wakati Sekta ya Ujenzi imekuwa kwa asilimia 14.1.

Ameongeza kuwa, wizara yake imekuwa ikikusanya kiasi cha wastani wa Shilingi bilioni 39 kwa mwezi lakini kwa mwezi Aprili makusanyo hayo yamepaa na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 58 jambo ambalo linaonesha mafanikio makubwa ya kisekta.

Waziri wa Madini, Doto Biteko

Hata hivyo, Waziri Biteko ametaka ukuaji huo wa Sekta ya Madini usaidie katika kukuza sekta nyingine za kiuchumi na hapo ndipo manufaa ya sekta ya madini yatakuwa na manufaa zaidi.  

Waziri Biteko amebainisha hayo leo Mei 18, 2020 alipokuwa akifungua warsha ya maandalizi ya kitabu cha viashiria hatarishi (Risk register) cha wizara inayofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa Chuo cha Madini Dodoma (MRI) na baadaye kuja na kitabu hicho kama matokeo ya warsha hiyo.

Biteko ameongeza kuwa, wizara inapoendelea kutekeleza majukumu yake, yumkini kuna viashiria hatarishi ambavyo endapo havitadhibitiwa vitakwamisha juhudi za wizara kufikia malengo, hivyo wizara imeamua kuandaa kitabu kitakachosaidia kubaini viashiria hivyo na kuvifanyia kazi ili kuyafikia malengo iliyojiwekea.

Akizungumza na washiriki wa warsha hiyo, Biteko amewataka wajumbe kubaini viashiria hatarishi vinavyoikabili wizara, kubuni mikakati madhubuti ya kudhibiti viashiria hivyo na kuandaa daftari la viashiria hatarishi la wizara kwa muda wa siku tano watakazokuwepo katika warsha hiyo.

Amesema, kwa kufanya hivyo, uhakika wa wizara pamoja na wadau wake wa malengo mkakati ya wizara kufikiwa utakuwa mkubwa kwani viashiria hatarishi vitakuwa vimepangiwa mikakati ya kuidhibiti kabla ya kutokea na kukwamisha juhudi za wizara.

Biteko amesema, maandalizi ya kitabu cha viashiria hatarishi ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa katika Waraka wa Hazina namba 12 wa mwaka 2013 ukielekeza taasisi zote za umma zikiwemo wizara kuwa na mfumo thabiti wa kudhibiti viashiria hatarishi (Risk Management) na kuandaa daftari la viashiria hatarishi (Risk register)

Ameendelea kusema suala la udhibiti na usimamizi wa viashiria hatarishi ilianzishwa mwaka 2010 kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho kati sura 348 ya Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001.

Waziri Biteko amesema usimamizi wa viashiria hatarishi kwenye taasisi za umma ni takwa la kisheria ambapo chimbuko lake ni marekebisho katika sura ya 348 ya Sheria ya Fedha za umma ya mwaka 2001 yaliyofanyika mwaka 2010 na hivyo kuanzishwa kwa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ambapo moja ya majukumu yake ni kusimamia mifumo ya udhibiti wa viashiria hatarishi vya malengo katika taasisi za umma.

Aidha, Waziri Biteko amewataka watendaji wa wizara kuendelea kuwakumbusha wachimbaji  na wafanyabiashara wa madini kuendelea kufuata sheria na taratibu zinazosimamia Sekta ya Madini ili iendelee kuzalisha kwa faida.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amewataka washiriki wote kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo ili kuvitambua viatarishi na kuviepuka kabla havijawa tatizo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *