TANZANIA YAANZA KUTEKELEZA MKAKATI WA KUFUFUA ZAO LA MCHIKICHI MKOA WA KIGOMA

Tanzania inaagiza asilimia 60 ya mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi kutokana na uhaba wa uzalishaji katika viwanda vilivyopo nchini.

Kufuatia hali hiyo Serikali ya Awamu ya Tano ilianza kutekeleza mkakati wa makusudi kwa kufufua zao la mchikichi katika Mkoa wa Kigoma ili kuwezesha uzalishaji wa mafuta na kuziba pengo la mafuta yanayoagizwa nje ya nchi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe . Kassim Majaliwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Kikosi cha 821 KJ Bulombora Kigoma Meja. Victor Faustine Rutayuga miche 163,000 inazalishwa ikiwa katika hatua mbalimbali, huku miche 26,800 ikiwa tayari kupandwa katika shamba la kikosi hicho kufikia mwezi Oktoba 2020 ili kutekeleza azma ya Serikali kuwezesha Taifa kujitegemea kwa mafuta ya kupikia.

Sehemu ya miche ya zao la mchikichi kama inavyoonekana katika kitalu cha uzalishaji wa miche hiyo katika Kikosi cha 821 KJ Bulombora Kigoma ambapo miche 163,000 inazalishwa ikiwa katika hatua  mbalimbali, huku miche 26,000 ikiwa tayari kupandwa katika shamba la kikosi hicho kufikia mwezi Oktoba 2020 ili kutekeleza   azma  ya Serikali kuwezesha Taifa kujitegemea kwa mafuta ya kupikia ambayo asilimia 60 kwa sasa inaagizwa kutoka nje ya nchi.


Akifafanua, Meja Rutayuga amesema kuwa kikosi hicho kimejipanga kikamilifu kutekeleza azma hiyo ya Serikali na tayari ekari 800 kati ya 2000 ziko tayari kupandwa miche mipya ambayo ni ya kisasa.

Alieleza kuwa mbegu hiyo ya kisasa aina ya Tenera itawezesha uzalishaji kuongezeka na kuziba pengo la uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mkuu wa Kikosi hicho, Meja Godfrey A. Mwakabole amesema kuwa dhamira ya Kikosi hicho ni kuzalisha miche zaidi ya mahitaji ya Kikosi na hivyo kuigawa kwa wananchi na Taasisi nyingine ili kuunga mkono azma ya Serikali kufufua zao hilo.

Aliongeza kuwa Kikosi hicho kinashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuhakikisha kuwa kinazalisha mbegu bora na kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Utafiti TARI Kihinga, Dkt. Filson Kagimbo amesema kuwa Kituo hicho kinafanya kazi kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Jeshi la kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza katika kuhakikisha kuwa azma ya Serikali inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Ad
Ad

Unaweza kuangalia pia

Uzinduzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya UCSAF Dodoma: Kuimarisha Mawasiliano Vijijini

25 Aprili 2024, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *