SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA SEKTA YA NISHATI KWA KASI

Na. Beatrice Saanga-MAELEZO

Nishati ni sekta muhimu sana kwa wananchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla hususani kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unazalishwa na  na kuwafikia wananchi walio wengi ili waweze kufikia ndoto zao za kuanzisha na kumiliki viwanda na kuweza kuinuka kuinua kipato cha familia zao na kuleta maendeleo ya nchi.

Ad

Aidha, nishati ya umeme inasalia kuwa muhimu sana katika maendeleo na ukuaji wa uchumi duniani kote  hasa kutokana na uhitaji mkubwa wa nishati  katika matumizi ya kila siku na  uzalishaji viwandani ambapo inahitajika katika kuendesha mitambo na mikubwa na katika viwanda vidogo vinavyomilikiwa na wajasiriamali wadogo.

Katika kipindi cha 2019/19, Wizara ya Nishati kwa imekuwa na vipaumbele vingi hasa katika kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unapatikana ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa nchi ambapo Serikali ya Rais John Pombe Magufuli imejitahidi kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji ambao ukikamilika utakuwa na  MW 2,100 uliopo wilayani Rufiji na miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I – Extension MW 185, Kinyerezi II MW 240, Somanga Fungu MW 330 ulioko mkoani Lindi pamoja na MW 300  ulioko katika mkoa wa Mtwara.

Aidha, Serikali imeimarisha  mifumo ya usafirishaji wa umeme mkubwa nchini ikiwa ni pamoja na  kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA), mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)  na kuendeleza miradi ya nishati jadidifu (jotoardhi, upepo na umeme-jua).

Jitihada za Serikali katika kuimarisha nishati zimeiwezesha kutekeleza miradi mingi ya kusafirisha umeme ambapo imepelekea kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta na kuwezesha kuokoa kiasi cha shilingi bilioni, 719 kwa mwaka. Mafanikio hayo yamewezekana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia 2019/20.

Wakati Tanzania inaelekea kutimiza azma ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa katika ya Mwaka 2025 Serikali kupitia, Wizara ya Nishati imelenga kuzalisha umeme wa MW 5,000, mwaka 2020 na kuongezeka hadi kufikia kufikisha MW 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Mahitaji ya umeme nchini yameendelea kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi zinazohitaji nishati ya umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye gharama nafuu pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa jumla ya MW 2,100 kwa kutumia maji (Hydro Power Plant) katika Bonde la Mto Rufiji ni kichocheo muhimu katika kuwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ampapo utekelezwaji wa mradi huu unategemewa kupunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la umeme nchini

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais  John Pombe Magufuli itahakikisha inasimamia ipasavyo na kuimarisha miundombinu ya nishati kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za umeme unaboreshwa ili kukabiliana na changomoto mbalimbali za uimarishaji wa Mikakati ya utoaji wa huduma ya nishati  ya Umeme.

Katika hotuba yake wakati wa akizindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma, tarehe, 13, Novemba 2020 Rais John Pombe Magufuli alisema Serikali yake inaenda kuwezesha upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijafikiwa na umeme na kuondoa kabisa tatizo la umeme vijijini.

“Kuhusu umeme pia, kwenye miaka mitano ijayo, tumepanga kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikishiwa umeme, ambapo idadi yake haizidi 2,384. Kwenye miaka mitano iliyopita, kwa takwimu za hadi jana tumefikisha umeme kwenye vijiji 9,884 kutoka vijiji 12,018 mwaka 2016. Nchi yetu ina vijiji 12,280”alisema Rais Magufuli.

Alibainisha kuwa kwenye miaka mitano ijayo Serikali yake imejipanga kukamilisha mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere ambalo linategemewa kuzalisha  megawati 2,115 ambapo Tanzania inakusudia kupata umeme wa kutosha kupitia mradi huo ambao unatarajiwa kupunguza bei ya umeme kwa wananchi.

Aliitaja miradi mingine ambayo Serikali inakusudia kuanza ujenzi wake katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miradi mingine ya umeme wa maji Ruhudji utakaokuwa na MW 358, Rumakali MW 222, Kikonge MW 300, umeme wa gesi Mtwara MW 300, Somanga Fungu MW 330,Kinyerezi III MW 600 na Kinyerezi IV MW 300. Aliongeza kuwa Serikali pia inakusudia kutekeleza miradi mingine midogo midogo ambayo kwa pamoja inakusudiwa kuzalisha umeme MW 1,100 kwa kutumia Nishati jadidifu (jua, upepo,jotoardhi)

Katika miaka mitano ijayo Serikali itakamilisha miradi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbali mbali ya nchini, hali itakayopelekea kuimalika kwa shughuli za viwanda,  kuongeza uzalishaji, pamoja na kupelekea kupanda kwa uchumi wa taifa pia Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani, kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiriko ya tabianchi. MWISHO

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tusikubali Kuwa Tarumbeta za Watu Wasio Tutakia Mema”

“Tusikubali kuwa tarumbeta za Watu wasio tutakia mema, Maadili Yetu Mazuri Ya Kitanzania Lazima Tuyatunze, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *