Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta nguo na mavazi ili kusikiliza changamoto wanazokutana nazo na mapendekezo yao katika kuboresha na kukuza sekta hiyo.
Akizungumza na wadau hao katika kikao kilichofanyika tarehe 9 Februari 2021 katika ukumbi wa Chuo cha Biashara (CBE ) jijini Dodoma Naibu Waziri aliwaagiza kuwasilisha changamoto walizonazo na rasimu za mipango mikakati ya kuboresha na kuendeleza Viwanda na Biashara katika sekta hiyo ili kukuza uchumi wa nchi.
Aidha katika kikao hicho kilichojumuisha wadau ambao ni watengenezaji na waagizaji wa nguo na mavazi kutoka nje ya nchi, wadau hao waliwasilisha changamoto na mapendekezo yao kwa Mhe. Naibu Waziri wakiwa na lengo la kuboresha na kukuza sekta hiyo.
Aidha, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuendeleza sekta ya nguo na mavazi nchini ikiwemo kukuza soko la ndani la.bidhaa hizo pamoja na kuandaa na kutekeleza Mkakati wa kuendeleza Sekta ya pamba nguo hadi mavazi ( Cotton to Clothing Strategy C2C 2016 – 2020 ) na kuuhuisha ambapo utekelezaji wake utaanza mwaka 2021 – 2032.