Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeliagiza Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuongeza juhudi na ubunifu katika utoaji wa huduma zinazotumia teknolojia ya kisasa ili kukuza viwanda vidogo na kuongeza ajira nchini.
Hayo, yalisemwa na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya SIDO na mafanikio yake iliyofanyika jana katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Aidha, Naibu Mwenyekiti huyo alisema SIDO inatakiwa kuongeza jitihada katika kufanya utafiti na ubunifu katika utengenezaji wa mitambo ya kisasa na inayokidhi mahitaji na kuafanyia kazi mawazo ya vijana wengi ambao ni wabunifu lakini hawana mitaji ya kuendeleza ubunifu wao.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira alisema Serikali inaendelea kuiwezesha SIDO kuboresha mitambo yake kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili iweze kuzalisha mitambo yenye ubora unaokidhi mahitaji na soko shindani la mitambo kutoka nje ya nchi.
Aidha, Alisema SIDO imeendelea kujenga mabanda (Industrial shades) katika kila mkoa yanayowawezesha wajasiliamali kuanzisha viwanda katika maeneo hayo kwa urahisi. Pia alisema SIDO imejipanga kutanua uwigo wa utuoaji huduma inayopatikana katika mikoa yote na sasa kuelekeza huduma hizo katika kila wilaya ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.
Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa na SIDO ikiwemo Matumizi ya TEHAMA, kutoa huduma bora kwa uadilifu na weledi kwa teknolojia ya kisasa, Kuanzisha vituo vya utafiti na ubunifu, kuongeza njia za kuwawezesha vijana wabunifu ili kuongeza ajira nchini na kuanzisha mpango wa kutoa Tuzo kwa vijana wabunifu.
Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji alisema SIDO inatoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia na viwanda hususani teknolojia za kuchakata mazao ya kimkakati kama Korosho; Alizeti, Mchikichi na nafaka katika vituo saba vya kuzalisha teknolojia ambavyo ni Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Moshi, Shinyanga na Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema huduma nyingine inayotolewa na SIDO ni kuendeleza ubunifu wa teknolojia kwa kutumia programu ya kiatamizi inayowalea, kuwapa mafunzo, kuwapa nafasi ya kufanyia kazi ndani ya eneo la SIDO bure na kuwaunganisha na taasisi za kifedha wajasiliamali wenye ubunifu wa teknolojia na mawazo ya bidhaa mpya kwa kipindi cha miaka mitatu . Programu hii huendeshwa katika vituo vinne (Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara na Iringa).
Aidha Alisema kuwa SIDO inashirikiana na TBS, TMDA, TRA na GPSA katika kutoa mafunzo kwa wajasiliamali katika ofisi za mikoa. Mafunzo yanayotolewa ni mafunzo ya ujasiliamali na mbinu za biashara, Mafunzo ya kiufundi na teknolojia na Mafunzo ya uhifadhi na usindikaji vyakula pamoja na kuwasaidia wajasiliamali hao kupata nembo za ubora kutoka TBS.
Pia alisema SIDO hutoa huduma za masoko kwa kuwashirikisha Wajasiriamali katika maonesho mbalimbali ya bidhaa na huduma yanayoandaliwa na Serikali kupitia SIDO au taasisi nyingine hapa nchini na nje ya nchi yakiwemo maonyesho ya kikanda na maonesho makubwa ya kitaifa.
Akiongelea huduma za kifedha zinazotolewa na SIDO , alisema mikopo hutolewa kwa wajasiliamali wenye viwanda vidogo kupitia mfuko wa “National Entrepreneurship Development Fund” (NEDF), Mfuko wa dhamana (CGS) na SANVN Viwanda Scheme ulioanzishwa kwa ushikiano wa SIDO, NSSF, VETA. ABL, na NEEC. SIDO inashirikiana na CRDB Bank kutoa mikopo kwa viwanda vinavyochakata mazao.
Aidha akitaja mafanikio ya SIDO kati ya mwaka 2016/17 – 2019/20, Mkurugenzi huyo alisema SIDO imefanikiwa kuanzisha Viwanda Vidogo sana 4,410, Viwanda vidogo 3,406 na Viwanda vya Kati 460. Pia alitaja baadhi ya viwanda vikubwa vilivyoanzia SIDO kuwa ni pamoja na Dabaga kilichopo mkoani Iringa, Mwanza Quality Wine kilichopo Mwanza, Tausi Coffee kilichopo Shinyanga na Mart Super Brand kilichopo Manyara
Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lilianzishwa kwa sheria namba 28 ya Bunge ya mwaka 1973 kwa lengo la Kushawishi, Kuhamasisha na Kusimamia uanzishwaji wa Viwanda Vidogo nchini, Kuongeza thamani ya raslimali zilizoko nchini, Kuwezesha kutengeneza bidhaa za kutosheleza mahitaji ya wananchi, Kuendeleza na kutumia teknolojia rahisi inayopatikana nchini, Kutoa kipaumbele kwa miradi ya uzalishaji inayotumia zaidi nguvukazi na Kutoa huduma kwa viwanda vidogo nchini