KAMATI YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA YAIAGIZA SIDO KUONGEZA JUHUDI NA UBUNIFU KATIKA UTOAJI WA HUDUMA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeliagiza Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuongeza juhudi na ubunifu katika utoaji wa huduma zinazotumia teknolojia ya kisasa ili kukuza viwanda vidogo na kuongeza ajira nchini.

Hayo, yalisemwa na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya SIDO na mafanikio yake iliyofanyika jana katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Ad
Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb ) akitoa maelekezo kwa SIDO kuongeza juhudi na ubunifu katika utoaji wa huduma ili kukuza viwanda na kuongeza ajira nchini katika semina ya kuwaelimisha wajumbe kuhusu Majukumu na Mafanikio ya SIDO iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Aidha, Naibu Mwenyekiti huyo alisema SIDO inatakiwa kuongeza jitihada katika kufanya utafiti na ubunifu katika utengenezaji wa mitambo ya kisasa na inayokidhi mahitaji na kuafanyia kazi mawazo ya vijana wengi ambao ni wabunifu lakini hawana mitaji ya kuendeleza ubunifu wao.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira alisema Serikali inaendelea kuiwezesha SIDO kuboresha mitambo yake kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili iweze kuzalisha mitambo yenye ubora unaokidhi mahitaji na soko shindani la mitambo kutoka nje ya nchi.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Cecil Mwambe akitoa maoni kuhusu SIDO kutoa huduma bora kwa teknolojia ya kisasa katika semina iliyotolewa na ili kuwaelimisha Kamati hiyo kuhusu Majukumu na Mafanikio ya SIDO iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Aidha, Alisema SIDO imeendelea kujenga mabanda (Industrial shades) katika kila mkoa yanayowawezesha wajasiliamali kuanzisha viwanda katika maeneo hayo kwa urahisi. Pia alisema SIDO imejipanga kutanua uwigo wa utuoaji huduma inayopatikana katika mikoa yote na sasa kuelekeza huduma hizo katika kila wilaya ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.

Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira  walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali  yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa na SIDO  ikiwemo  Matumizi ya TEHAMA, kutoa huduma bora  kwa uadilifu na weledi kwa teknolojia ya kisasa, Kuanzisha vituo vya utafiti na ubunifu, kuongeza njia za kuwawezesha vijana wabunifu ili kuongeza ajira nchini na kuanzisha mpango wa kutoa Tuzo kwa vijana wabunifu.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akijumuisha maoni na mapendekezo kuhusu uboreshaji na utoaji wa huduma za SIDO kwa kutumia teknolojia ya Kisasa katika semina ya kuwaelimisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira kuhusu Majukumu na Mafanikio ya SIDO iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji  alisema SIDO inatoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia na viwanda   hususani teknolojia za kuchakata  mazao ya kimkakati  kama Korosho; Alizeti, Mchikichi na nafaka katika  vituo saba vya kuzalisha teknolojia ambavyo ni Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Moshi, Shinyanga na Kigoma.

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema huduma nyingine inayotolewa na SIDO ni kuendeleza ubunifu wa teknolojia kwa kutumia programu ya kiatamizi inayowalea, kuwapa mafunzo, kuwapa nafasi ya kufanyia kazi ndani ya eneo la SIDO bure na kuwaunganisha na taasisi za kifedha  wajasiliamali wenye ubunifu wa teknolojia na mawazo ya bidhaa mpya kwa kipindi cha miaka mitatu . Programu hii huendeshwa katika vituo vinne (Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara na Iringa).

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Dkt Charles Kimei akitoa maoni kuhusu uboreshaji wa huduma zinazotolewa na SIDO kwa kutumia TEHAMA katika semina iliyotolewa na ili kuwaelimisha Kamati hiyo kuhusu Majukumu na Mafanikio ya SIDO iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Aidha Alisema kuwa SIDO inashirikiana na TBS, TMDA, TRA na GPSA katika kutoa mafunzo kwa wajasiliamali katika ofisi za mikoa. Mafunzo yanayotolewa ni mafunzo ya ujasiliamali na mbinu za biashara, Mafunzo ya kiufundi na teknolojia na Mafunzo ya uhifadhi na usindikaji vyakula pamoja na kuwasaidia wajasiliamali hao kupata nembo za ubora kutoka TBS.

Pia alisema SIDO hutoa huduma za masoko kwa kuwashirikisha Wajasiriamali katika maonesho mbalimbali ya bidhaa na huduma yanayoandaliwa na Serikali kupitia SIDO au taasisi nyingine hapa nchini na nje ya nchi yakiwemo maonyesho ya kikanda na maonesho makubwa ya kitaifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji akiwaelimisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika semina iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Akiongelea huduma za kifedha zinazotolewa na SIDO , alisema mikopo hutolewa kwa wajasiliamali wenye viwanda vidogo kupitia mfuko wa “National Entrepreneurship Development Fund” (NEDF), Mfuko wa dhamana (CGS) na SANVN Viwanda Scheme ulioanzishwa kwa ushikiano wa SIDO, NSSF, VETA. ABL, na NEEC. SIDO inashirikiana na CRDB Bank kutoa mikopo kwa viwanda vinavyochakata mazao.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira wakisikiliza kwa makini wasilisho kuhusu Majukumu na Mafanikio ya SIDO katika semina iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma

Aidha akitaja mafanikio ya SIDO kati ya mwaka 2016/17 – 2019/20, Mkurugenzi huyo alisema SIDO imefanikiwa kuanzisha Viwanda Vidogo sana 4,410, Viwanda vidogo 3,406 na Viwanda vya Kati 460. Pia alitaja baadhi ya viwanda vikubwa vilivyoanzia SIDO kuwa ni pamoja na Dabaga kilichopo mkoani Iringa, Mwanza Quality Wine kilichopo Mwanza, Tausi Coffee kilichopo Shinyanga na Mart Super Brand kilichopo Manyara

Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lilianzishwa kwa sheria namba 28 ya Bunge ya mwaka 1973 kwa lengo la Kushawishi, Kuhamasisha na Kusimamia uanzishwaji wa Viwanda Vidogo nchini, Kuongeza thamani ya raslimali zilizoko nchini, Kuwezesha kutengeneza bidhaa za kutosheleza mahitaji ya wananchi, Kuendeleza na kutumia teknolojia rahisi inayopatikana nchini, Kutoa kipaumbele kwa miradi ya uzalishaji inayotumia zaidi nguvukazi na Kutoa huduma kwa viwanda vidogo nchini

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mitazamo ya Uongozi ya Mhe. Ummy Ally Mwalimu katika Sekta za Afya, Maendeleo ya Jamii, na Haki za Watoto

Ummy Ally Mwalimu ameonyesha mitazamo ya uongozi yenye mwelekeo wa kujali maendeleo na ustawi katika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *