WAZIRI MHAGAMA AIOGONZA KAMATI KUDUMU YA BUNGE PAC KUUKAGUA MRADI WA MBIGIRI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameiongoza kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC) kuukagua mradi wa uzalishaji sukari katika shamba la Mbigiri,  wilayani kilosa mkoani Morogoro.

Akiongea wakati wa kikao na Kamati hiyo aliihakikishia kuwa nia ya serikali ya Awamu ya Tano ni kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kuweza kupunguza naksi ya mahitaji ya sukari nchini pamoja na kuweza kutengeneza ajira za moja kwa moja na ajira zisizokuwa za moja kwa moja kwa watanzania.

Ad

Mradi huo kwa sasa umeajiri moja kwa moja wafanyakazi 387. Kati ya hao, 300 ni vibarua katika mashamba. Inakadiriwa kwamba mradi  tayari umetoa ajira ambazo si za moja kwa moja kwa wananchi zaidi ya 2,000.

Uzalishaji wa sukari utakapoanza jumla ya wananchi zaidi ya 1,200 wataajiriwa, kati ya hao 650 watakuwa mashambani. Pia ajira zisizokuwa za moja kwa moja kwa wananchi zaidi ya 5,000 zitapatikana. Aidha, kwa sasa kilimo cha miwa kwa wakulima wa nje zaidi ya 245 wamehamasishwa na wakulima 1, 000 wanatarajiwa kuwa wamehamasishwa kiwanda kitakapoanza uzalishaji sukari.

Mradi huo unaotarajiwa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka, unatarajia kuanza kuzalisha sukari kwenye kiwanda cha Mbigiri katika kipindi cha mwisho  wa msimu wa  mwaka 2021/2022 ambapo maandalizi ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda yamefanyika kwa kutenga eneo la ukubwa wa hekta 35.3.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC), Mhe. Naghenjwa Kaboyoka aliwaongoza wajumbe wa kamati hiyo kukagua eneo lililotengwa kwa ajili  ya ujenzi wa kiwanda, mabweni kwa ajili ya mafundi 112 wa awali wa kiwanda, ofisi za kiwanda, ukumbi mdogo wa mikutano, barabara ya kuelekea eneo la kiwanda pamoja na bwawa la kuhifadhi maji ya kumwagilia miwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya Mradi Dkt. Hildelitha Msita, ameeleza kuwa mradi umejenga zahanati itakayotumiwa na wafanyakazi pamoja na wananchi wanaoishi jirani na mradi. Aidha, ameeleza kuwa wanaendelea kuboresha kazi za kilimo kwa kununua zana za kilimo na vifaa vya kisasa vya kilimo kulingana na mpango mkakati. Lengo la mradi ni kufikia uzalishaji wa sukari kiwango cha tani 110 kwa hekta ifikapo mwaka 2021/2022  na tani 130 kwa hekta ifikapo mwaka 2023/2024.

Kampuni Hodhi ya Mkulanzi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha jumla 250,000 za sukari kwa mwaka ili kupunguza nakisi ya mahitaji ya sukari nchini. Endapo Mradi wa Mbigiri Estate, ukianza kutekelezwa unatarajia kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.Uzalishaji huo utasaidia kupunguza naksi ya mahitaji ya sukari nchini. Kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia tisini na sita na Shirika la Uzalishaji mali Magereza kwa asilimia nne.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *