RAIS SAMIA AONGOZA VIONGOZI WA NDANI NA NJE YA NCHI KUMUAGA ALIYEKUWA RAIS WA TANZANIA HAYATI DKT. MAGUFULI, JIJINI DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa na Viongozi wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa mbalimbali Duniani kwenye Mazishi ya Kitaifa ya kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma leo March 22,2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 22 Machi, 2021 amewaongoza Watanzania, Wakuu wa Nchi na Serikali,  wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na viongozi mbalimbali kutoa heshima za mwisho Kitaifa kwa mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Rais Samia amewashukuru Waheshimiwa Marais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wawakilishi wa Wakuu wa Nchi waliokuja kuungana na Watanzania katika kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dkt. Magufuli na ameeleza kuwa ujio wao na jinsi Watanzania walivyoonesha mapenzi yao tangu msiba huu mkubwa wa Kitaifa utokee vimedhihirisha kuwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa kipenzi cha watu.

Ad
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Viongozi wa Mataifa ya Nchi mbalimbali Duniani na Wananchi wa Jiji la Dodoma kwenye Mazishi ya Kitaifa ya kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma leo March 22,2021.

Mhe. Rais Samia amesema Hayati Dkt. Magufuli alikuwa mwalimu, kiongozi na mlezi wake na kwamba alihusudu utendaji wake kwa namna alivyokuwa mfuatiliaji na msimamizi wa miradi.

Amebainisha kuwa Taifa limepoteza kiongozi mahiri, shupavu, jasiri, mchapakazi, muadilifu, mnyenyekevu, mcha Mungu, mfuatiliaji, mzalendo kwa Taifa lake, mtetezi wa wanyonge, mwanamwema wa Afrika, mwanamageuzi mahiri, mwanamapinduzi wa kweli, mtu asiyekuwa na makuu na mtumishi wa wote.

Mama Janeth Magufuli Mjane wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli akilia kwa uchungu wakati akitoa Heshima za mwisho kwenye Jeneza la mme wake katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa wakati wa uongozi wake, Hayati Dkt. Magufuli aligusa maisha ya watu wengi na kwa muda mfupi, na kwamba kwa kipindi alicholiongoza Taifa alijikita kujenga uchumi wa ndani unaotegemea mapato ya ndani, kusimamia rasilimali za Taifa ili zifaidishe wananchi kwa kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato, kufufua na kuwekeza katika miradi ya kimkakati kama vile kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) kwa kununua ndege na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway – SGR) ili kufanikisha azma ya ujenzi wa viwanda ambavyo vinahitaji miundombinu wezeshi.

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa Heshima za Mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zimbabwe Mhe. Emmason Mnangagwa akitoa Heshima za Mwisho kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Mazishi ya Kitaifa yaliyofanyika leo March 22,2021 katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma.

Amesema katika kipindi chake cha uongozi, Tanzania ilipata Makamu wa Rais mwanamke ambaye leo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amewahakikishia Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa yeye na viongozi wenzake wapo tayari kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kwamba yale aliyoyakusudia yatafikiwa.

Mhe. Rais Samia amewaondoa shaka walio na wasiwasi juu ya hatma ya Tanzania baada ya Hayati Dkt. Magufuli kufariki dunia kuwa kila kitu kitakuwa sawa “Kwa wale ambao wana mashaka mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”

Rais wa Jamhuri ya Watu wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta akitoa Heshima za Mwisho kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Mazishi ya Kitaifa yaliyofanyika leo March 22,2021 katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma.

Amewataka Watanzania kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli kwa kutekeleza yote mazuri aliyoyafanya katika ujenzi wa Taifa.

Ameihakikishia familia ya Hayati Dkt. Magufuli kuwa Taifa linatambua mchango mkubwa ambao ameutoa na kwamba atakuwa nao na kuwashika mkono siku zote.

Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zambia Mhe. Edgar Lungu akitoa Heshima za Mwisho kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Mazishi ya Kitaifa yaliyofanyika leo March 22,2021 katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbuji Mhe. Filipe Nyusi akitoa Heshima za Mwisho kuaga Mwili wa aliyekuwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Mazishi ya Kitaifa yaliyofanyika leo March 22,2021 katika Uwanja wa Jamhuri JIjini Dodoma.

Mhe. Rais Samia amewahakikishia nchi marafiki na majirani wa Tanzania kuwa Tanzania itaendelea kuwa jirani mwema na mshirika mzuri katika ushirikiano wa kikanda na kimataifa, na kwamba uhusiano wake utaimarika zaidi katika kipindi chake cha uongozi.

Katika salamu zao, Marais 9 wa nchi mbalimbali za Afrika wamemshukuru Hayati Dkt. Magufuli kwa utumishi wake wakati wa uhai wake ambapo alionesha mfano wa namna Afrika inavyoweza kujiamulia mambo yake yenyewe, kujitegemea, kujenga uchumi wake, kupiga vita rushwa na kuwapigania watu wake.

Maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakisindikiza Jeneza lenye Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuliweka kwenye Sehemu  maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya Viongozi wa Mataifa mbalimbali Dunia na Wananchi wa Jiji la Dodoma kuweza kutoa Heshima zao za Mwisho kuaga Mwili wa Kiongozi huyo leo March 22,2021 katika uwanja wa Jamhuri jijini dodoma. (Picha na Ofisi ya Rais)

Wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wamemhakikishia ushirikiano na uhusiano mzuri katika kipindi chote cha uongozi wake.

Dkt. John Pombe Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi, 2021 Jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo na atazikwa tarehe 26 Machi, 2021 nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *