- Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi jana (Oktoba 31) alitembelea mradi wa ujenzi wa meli ya kisasa ambayo ni meli kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na ujenzi wa chelezo kwa ajili ya matengenezo na marekebisho ya meli mbalimbali ikiwa ni uwekezaji unaofanywa na Serikali.
- Akiwa katika eneo hilo, Dkt. Abbasi alisema kuwa ujenzi wa meli mpya ni ahadi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 23 iliyopita, ambayo imetekelezwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.
- Aidha, Dkt. Abbasi aliongeza kuwa ujenzi wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200 umefikia asilimia 33 ya ujenzi na utakamilika mapema mwaka 2021, ambapo Serikali imewekeza zaidi ya TZS Bilioni 150, kwenye mradi ya meli pamoja na ujenzi wa chelezo.
- Aidha, Dkt. Abbasi alishuhudia ukarabati unaoendelea katika meli ya MV. Victoria, ambayo baada ya kukamilika itasaidia kutoa huduma bora za usafiri kwenye eneo la Ziwa Victoria.
- Vilevile, akiwa ziarani hapo Dkt. Abbasi alisema kuwa ipo miradi mingi kwenye eneo la Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, inatakayo gharimu zaidi ya TZS Bilioni 300.
- Aliongeza kuwa hivi karibuni, Serikali itasaini makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa meli katika eneo la Ziwa Tanganyika na uundaji wa meli 3 mpya na za kisasa katika eneo la Ziwa Nyasa.
- Akitaja, meli zilizokamilika kutokana na utekelezaji wa ahadi za Serikali hadi sasa kuwa ni meli za mbili za mizigo za MV. Ruvuma, na meli kubwa ya kisasa ya abiria ya MV. Mbeya II na ambayo tayari imeanza kazi.
- Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Eric Hamissi, alisema kuwa ujenzi wa meli hiyo mpya unaendelea vizuri, na Septemba 30, mwaka huu vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa vilianza kuletwa na sasa kazi ya uunganishwaji wa vyuma imeshaanza.
- Aliongeza kuwa, ujenzi wa chelezo umefikia 53%, na ifikapo Machi mwakani chelezo itanza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya.
- Aidha, Bw. Hamissi alisema anaishukuru Serikali kwa ujenzi miradi hii miwili pamoja na ya ukarabariti wa MV. Butiama na MV. Victoria inayoendelea kwani itaigharimu Serikali TZS Bilioni 150, na hadi sasa Serikali imeshatoa TZS Bilioni 70.8, sawa na 47% ya miradi yote minne.
- Bw. Hamissi, aliongeza kuwa miradi hii imesaidia kukuza uchumi wa Mwanza kwa kutoa ajira zaidi ya watu 1,000 pamoja utumiaji wa malighafi na watoa huduma, hali inayosaidia kuboresha maisha ya wananchi.
- Alifafanua kuwa, huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ambao haujawahi kutokea tangu Uhuru na ni mapinduzi katika usafiri wa njia ya maji kwa kutekeleza miradi mikubwa minne kwa wakati mmoja, na kuwa awali meli nyingi zilijengwa kwa msaada mfano MV. Sangara.
- Naye, Li Yonjee, Mtaalamu wa Meli kutoka Korea Kusini, alisema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa fursa ya kushiriki katika uundaji wa meli mpya ya kisasa, watatumia ujuzi wao wa uundaji wa meli waliofanya katika nchi za Korea ya Kusini, China na Japan, zikiwa ndio nchi kubwa za uundaji wa meli duniani, katika kuunda meli mpya ya Tanzania.
- Vilevile, Bw. Li alisema kuwa wanaahidi kutimiza matarajio ya Serikali na watanzania kwa ujumla kwa kuunda meli hiyo kwa mafanikio, pamoja kuikamilisha kwa wakati.
- Aidha, Bhoke Siguta mwanamke anayefanyakazi ya kuchomelea vyuma katika mradi wa uundaji wa meli mpya, alisema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa maisha ya watanzania, ikiwemo kutoa ajira.
- Bi. Siguta alisisitiza kuwa, kupitia mradi huu wa uundaji wa meli mpya ameweza kupata ajira, inayompatia kipato cha kumsaidia kutunza familia yake.
- Pia, ameshauri wanawake kujishughulisha na kazi za uchomeleaji vyuma, kwani ni kazi nzuri na zitawajengea uwezo zaidi wa kujiamini pamoja na kukuza kipato.
- Awali, Dkt. Abbasi alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Huduma za Meli kuhusu mikakati na maboresho ya kampuni hiyo.
Ad