Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayolenga kudumisha zaidi ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia na biashara. Vilevile wamejadili kuhusu ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi na programu mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China ili kuhakikisha zinaleta tija kwa manufaa ya pande zote mbili.
Balozi Ibuge kwa upande wake ameeleza kuwa kuwepo kwa uhusiano mzuri wa Kidiplomasia baina ya Tanzania na China kumechagiza kwa kiasi kikubwa kukuwa kwa biashara, utali na uwekezaji baina ya nchi hizi mbilia hivyo urafiki na undugu kati ya Mataifa haya mawili unapaswa kulindwa, kudumisha na kuendelezwa siku zote na katika hali yoyote. “China kwa muda mrefu imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Taifa letu kupitia sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa mundombinu ya usafirishaji na mawasiliano kama vile reli na barabara, hivyo Wizara na Serikali kwa ujumla inadhamini na kulinda undugu huu wa kihistoria” Balozi Brigedia Jenerali Wiibert A. Ibuge
Balozi Wang Ke kwa upande wake ameshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa akiendelea kuupata kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha serikali za nchi hizi mbili na watu wake wananufaika kotokana na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo.