UJERUMANI YATOA MSAADA WA SH. BILIONI 330 KWA AJILI YA MRADI WA MAJI MKOA WA SIMIYU

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
  • Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya  Maendeleo (KfW), imeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 127.7, sawa na sh. bilioni 330, kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria katika mkoa wa Simiyu.
  • Makubaliano ya msaada huo kupitia mikataba miwili yamesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani, (KfW) anayeshughulikia nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya, Dkt. Klaus Mueller.
KM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) katika nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya Dkt. Klaus Mueller, wakisaini Mkataba wa msaada wa Euro milioni 127.7 sawa na Sh. bilioni 330 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji kutoa Ziwa Victoria kupitia mradi wa kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia nchi katika Mkoa wa Simiyu, hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
  • Katika mkataba wa kwanza, kiasi cha Euro 102.7, sawa na shilingi bilioni 265 kimetolewa na Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi (Green Climate Fund) na mkataba wa pili unahusisha Euro milioni 25, sawa na sh. bilioni 65 ambazo zimetokelewa na Benki ya Maendeleo ya UJerumani (KfW).
  • Mbali na mradi wa maji  wa Simiyu ambao chanzo chake cha maji ni kutoka Ziwa Victoria, miradi mingine itakayonufaika na msaada huo ni kilimo endelevu cha umwagiliaji, usafi wa mazingira, maji na malisho ya mifugo na kuzijengea uwezo taasisi zitakazotekeleza mradi huo hasa mamlaka za maji katika Wilaya tano za Bariadi, Itilima, Meatu, Busega na Maswa zitakazonufaika na mradi huo.
 

KM

  • “Kutokana na umuhimu wa mradi huo wa maji, Serikali kwa upande wake itachangia Euro milioni 40.7 sawa na sh. bilioni 104 na wananchi watakao nufaika na mradi huo watachangia Euro milioni 1.5 sawa na sh. bilioni 3.8 na kufanya gharama za mradi mzima kufikia zaidi ya Euro milioni 171 sawa na zaidi ya sh. bilioni 446” alisema Bw. Doto James
  • Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Mfuko wake wa Kimataifa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (GCF) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha kitakachotumika kutekeleza mradi huo utakachukua miaka mitano hadi kukamilika kwake.
 
KM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), akieleza kuwa licha ya msaada wa Sh. bilioni 330 kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW), kwa ajili ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika Mkoa wa Simiyu, Serikali ya Tanzania itachangia kiasi cha Euro milioni 40.7 ambayo ni sawa na Sh. 104.1 kutokana na umuhimu wa mradi huo.
  • “Katika kipindi cha miaka  mitatu Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania zaidi ya Euro 202.8 sawa na shilingi bilioni 518.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, nishati, uhifadhi wa maliasili, udhibiti wa fedha za umma na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi” alisisitiza Bw. James
  • Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya KfW amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Mfuko wa Kimataifa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutoa kiasi kikubwa cha fedha cha Euro milioni 102.7 kwa mkupuo katika nchi za kiafrika tangu mfuko huo uanzishwe.
KM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo (kushoto), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mahamouud Mgimwa (Mb)(wapili kushoto), Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedhja na Mipango Bw. John Rubuga (wa pili kuli) na Kamishna wa Sera wa Wizara hiyo Bw. Mgonya Benedicto wakiwa katika hafla ya utiwaji saini mikataba miwili yenye jumla ya kiasi cha Euro milioni 127.7 sawa na Sh. bilioni 330 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji katika Mkoa wa Simiyu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
  • “Tunaamini kuwa zaidi ya watu 500,000 watanufaika na mradi huu wa maji kutoka Ziwa Victoria unaohusiana na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kutuhifadhi vyanzo vya maji, usafi wa mazingira, kuendesha kilimo bora chenye kuhifadhi mazingira” aliongeza Dkt. Mueller.
KM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo, akieleza kuwa Euro milioni 127.7 sawa na Sh. bilioni 330 zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) zitawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Simiyu kupitia miradi ya maji, kilimo cha umwagiliaji na usafi wa mazingira, wakati wa hafla ya kusaiiniwa kwa msaada wa fedha hizo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
  • Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo, amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuipatia Wizara yake zaidi ya shilingi trilioni 3 katika kipindi kifupi cha miaka mili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji inayoendelea kujengwa nchini kote.
 
KM-6
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Mahamoud Mgimwa (Mb), akieleza kuwa msaada wa Sh. bilioni 330 zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi utasaidia kuondoa malalamiko ya mda mrefu ya wabunge wa wilaya zitakazonufaika na mradi huo kuhusu ukosefu wa maji Mkoa wa Simiyu.
  • Alitaja sababu za mkoa wa Simiyu kunufaika na msaada huo kuwa ni mkoa unaokabiliwa na hali mbaya ya hewa ukiwemo ukame na kwamba mradi huo utawawezesha wananchi kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kwamba katika ukanda huo wa Ziwa kutakuwa na miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.2 itakayokuwa inatekelezwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati) na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) katika nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya Dkt. Klaus Mueller (wa pili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Benki ya KfW ya Ujerumani baada ya kukamilika kwa hafla ya kusainiwa mkataba wa msaada wa Euro milioni 127.7 sawa na Sh. bilioni 330 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji kutoa Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu.
  • Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Mahamoud Mgimwa amesema Bunge litahakikisha linausimamia mradi huo utekelezwe kwa wakati kwa sababu Serikali imedhamiria kwa dhati kuona kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
Ad

Unaweza kuangalia pia

NCHI ZA SADC ZATAKIWA KUTATHMINI UCHUMI WAKE BILA KUTEGEMEA MASHIRIKA YA KIMATAIFA PEKEE

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa nchi za Afrika hasa zilizopo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *