HATUTAONGEZA MUDA – DKT KALEMANI

 • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekataa maombi ya mkandarasi kampuni ya KEC International Ltd kutoka India, anayetekeleza mradi wa kupanua kituo cha kupoza umeme kilichopo Zuzu, mkoani Dodoma, kuongezewa miezi mitatu zaidi ili akamilishe kazi hiyo.
 • Badala yake, Dkt Kalemani amemtaka Mkandarasi huyo kukamilisha kazi husika na kuikabidhi kabla ya Januari 28, mwakani kama ilivyo kwenye mkataba wake.
 • Waziri alitoa msimamo huo Novemba 4, 2019 alipofanya ziara katika Kituo hicho kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi husika.
1-01
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu-kushoto), akitoa maelekezo kwa viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), alipofanya ziara katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Zuzu, mkoani Dodoma, Nov 4, 2019.
 • “Tumia mbinu zote unazozijua ikiwemo kuongeza wafanyakazi na kufanya kazi usiku na mchana, ilimradi ukamilishe kazi kwa wakati ulioanishwa katika mkataba. Sisi hatutakuongeza muda hata siku moja,” alisisitiza Waziri.
 • Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara yake, Waziri aliwaeleza kuwa kazi ya kupanua kituo hicho itakapokamilika, itakiwezesha kuongeza megawati 600 za umeme kutoka 48 zilizopo sasa, hivyo kuwa na jumla ya megawati 648.
 • Alisema, ongezeko hilo litawezesha kuwepo na umeme wa uhakika kwa wananchi wa jiji la Dodoma ambalo linakua kwa haraka na ni Makao Makuu ya Serikali.
 • “Mkoa wa Dodoma unatakiwa uwe na umeme mwingi sana. Kwa sasa kituo kinazalisha megawati 48, lakini tangu tumehamia hapa mwaka juzi, mahitaji yamekuwa yakiongezeka kutoka megawati 15 hadi 28 mwaka jana, na sasa tunapoongea yamefikia takribani megawati 33. Kwahiyo, umeme uliobaki siyo mwingi.”
 • Aidha, Waziri alitoa maelekezo kwa Msimamizi wa Kituo hicho, kuhakikisha vifaa vilivyopata hitilafu vinabadilishwa ndani ya siku hiyo aliyofanya ziara ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika.
2-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake (kushoto), wakikagua maendeleo ya ujenzi kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, mkoani Dodoma Nov 4, 2019.
 • Aliwataka kujenga utaratibu wa kukagua vifaa mbalimbali katika Kituo hicho na kuvibadilisha kwa wakati badala ya kusubiri hadi vinapata hitilafu na kusababisha changamoto ya upatikanaji umeme kwa wananchi.
 • Katika hatua nyingine, Waziri alitembelea mitaa mbalimbali ya Maungu, jijini Dodoma, ambayo haijaunganishiwa umeme ili kujionea hali halisi na kutoa miezi sita kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha upelekaji wa umeme katika maeneo yote ya jiji ambayo hayajafikiwa.
 • Aidha, aliwaagiza kuhakikisha wanawatembelea wananchi ambao maeneo yao yamefikiwa na umeme lakini bado hawajalipia, ili wawape elimu ya umuhimu wa kulipia na kuunganishiwa umeme.
 • Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Veronica Simba – Dodoma
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *