MRADI WA KIWANDA KIKUBWA CHA DAWA TANZANIA WAVUTIA WAWEKEZAJI WA KIMKAKATI AFRIKA KUSINI

BB 5-01
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kulia) akizungumza na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Alex Mubiru, kando ya Kongamano la Jukwaa la Wawekezaji Afrika (Africa Investment Forum), unaoendelea Mjini Johannesburg, Afrika Kusini
  • Tanzania imewasilisha miradi 13 ya Kipaumbele kwa wawekezaji wa kimkakati wanaoshiriki kongamano la Jukwaa la Uwekezaji Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
  • Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango anayemwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Jukwaa hilo, amesema Mradi wa Ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa  mchanganyiko kitakachogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 408 umewavutia wawekezaji wengi.
BB 2-01
Mkuu wa Idara ya Huduma za Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Abubakar Ndwata, akimweleza mwekezaji kutoka Kampuni ya Burhani Engineers kutoka Zoher Pirbhai kutoka nchini Kenya kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania, wakati wa Kongamano la Jukwaaa la uwekezaji la Afrika, linalofanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini,
  • Amewataja wawekezaji waliovutiwa na mradi  wa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachojengwa Kibaha mkoani Pwani, kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya aina 230 za dawa kwamba wanatoka nchi za Korea, Uturuki, taasisi za fedha za kimataifa na kwamba hadi kufika mapema mwakani (2020) mwekezaji mmoja au zaidi watakuwa wamepatikana kwa ajili ya kuanza kujenga mradi huo.
  • “Pamoja na kupunguza tatizo la uhaba wa dawa na dawa bandia zinazoingizwa nchini, kiwanda hiki pia kitazalisha ajira  kwa watanzania” alisema Dkt. Mpango.
BB 3-01
Baadhi ya wawekezaji wa kimkakati kutoka nchini Korea, Uturuki na Taasisi za Fedha za Kimataifa, wakielezea nia yao ya kuwekeza kwenye Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha dawa nchini Tanzania unaotarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 408, walipokutana na kufanya kikao na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, mjini Johannesburg, Afrika Kusini
  • Dkt. Mpango amesema Serikali inatenga zaidi ya sh bilioni 230 kwenye Bajeti kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa huku mahitaji halisi ya dawa nchini ni takriban shilingi trilioni 1.4 ndio maana mkazo umewekwa kwenye ujenzi wa kiwanda hicho kitakachotatua changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.
  • Alifafanua kuwa miradi mingine 12 iliyowasilishwa mbele ya wawekezaji hao iko katika hatua za maandalizi na iko katika sekta za Nishati ya umeme unaotumia nguvu ya maji, viwanda vya kuchakata pamba ili kuiongezea thamani na hatimaye kuzalisha nguo, ambavyo vinaendana na dhamira ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
  • Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka Bohari ya Dawa ya Taifa Mhandisi Fredrick Pondamali ameeleza kuwa usanifu wa mradi huo wa kiwanda cha kuzalisha dawa mchanganyiko umekamilika pamoja na viwanda vingine viwili zaidi vinavyotafutiwa wawekezaji.
BB4-01
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (aliyeipa mgongo kamera kushoto) akizungumza na wawekezaji wa kimkakati walioonesha nia ya kuwekeza kwenye Mradi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa chenye thamani ya dola za Marekani milioni 408, kutoka nchi za Korea, Uturuki na taasisi za fedha za kimataifa, wakati wa Jukwaa la Africa Investment Forum), unaoendelea Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
  • Alisema kuwa mradi wa kiwanda cha kuzalisha dawa ulichaguliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa lengo la kuupeleka mbele ya wawekezaji ili uweze kupata fedha kutokana na umuhimu wake kwa Tanzania na nchi jirani.
  • Jukwaa hilo la Uwekezaji Afrika linalofanyika kwa mwaka wa pili sasa limeandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali ambapo mwaka huu limevuta wawekezaji wa kimkakati zaidi ya 2000 kutoka kila pembe ya dunia ikiwa na lengo la kuongeza uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi katika nchi za Bara la Afrika.Na Benny Mwaipaja, Johannesburg
Ad

Unaweza kuangalia pia

TRA – WAFANYABIASHARA MSIJIHUSISHE NA BIASHARA ZA MAGENDO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara na wachuuzi wanaoishi jirani na fukwe za Bahari …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *