TRA YANG’ARA TUZO ZA NBAA, YAPATA USHINDI WA JUMLA

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshinda tuzo mbili ikiwemo mshindi wa jumla katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu mwaka 2018 kwa kufuata viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Taasisi za Umma yaani mfumo wa IPSASs.
2-01
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akionyesha tuzo ya mshindi wa kwanza ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu katika kipengele cha Wakala wa Serikali aliyopokea kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamis Shaabani wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam.
  • Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam, TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwenye kipengele cha Wakala wa Serikali na mshindi wa jumla kwa taasisi, wakala, kampuni na mashirika mbalimbali ambayo yamefanya vizuri katika kuandaa taarifa za fedha katika shughuli zao za kila siku.
  • Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Edwin Mhede, ameipongeza Idara ya Fedha na idara nyingine ndani ya mamlaka hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa tuzo hizo.
3-01
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede (katikati aliyeshika tuzo) akiwa na Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo (wa pili kushoto kwake) pamoja na watumishi wa Idara ya Fedha mara baada ya kupokea tuzo mbili za uandaaji bora wa taarifa za hesabu wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam.
  • “Nachukua nafasi hii kumshukuru mkuu wa idara anayehusika na Idara ya Fedha pamoja na wakuu wa idara nyingine ndani ya mamlaka maana zote zinatoa mchango mkubwa kuhakikisha idara hii inatoa taarifa sahihi na zenye kuleta mipango sahihi kwa mamlaka na serikali kwa ujumla,” alisema Dkt. Mhede.
  • Dkt. Mhede alieleza kuwa, taarifa sahihi ni msingi wa mipango kwa kuwa taasisi isiyopanga kushinda ni sawa na taasisi inayopanga kushindwa hivyo suala la uandaaji bora wa taarifa za hesabu ni moja ya ufanisi wa ofisi yoyote hapa ulimwenguni.
  • Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) ndio hutoa tuzo hizo kila mwaka ambapo mwaka 2017 TRA iliibuka mshindi wa kwanza tena katika uandaaji bora wa taarifa za hesabu katika kipengele cha Wakala wa Serikali. Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAKAZI WA PEMBEZONI MWA BAHARI WAELIMISHWA ATHARI ZA MAGENDO

Wakazi na wafanyabiashara waishio pembezoni mwa fukwe za Bahari ya Hindi katika kata za Somangila, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *