MRADI WA MAJI WA BIL 9.4 KYAKA – BUNAZI WASAINIWA

Mhandisi Mradi wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi He Jun (kushoto) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka-Bunazi. Wengine ni watendaji kutoka MWAUWASA.

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) ya China kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka- Bunazi wenye thamani ya shilingi 9,414,739,257.50.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba huo kwenye Ofisi za MWAUWASA, Jijini Mwanza, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele aliipongeza kampuni hiyo kwa kushinda tenda na alibainisha kwamba ujenzi wa mradi huo utachukua miezi 13.

Alisema mkataba unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji kwenye Mto Kagera chenye uwezo wa kuzalisha lita za maji 6,574,000 kwa siku; ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya maji; ujenzi wa kituo cha tiba ya maji kitakachokuwa na tenki la kuhifadhia maji.

Alibainisha kwamba kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Kyaka, Bunazi na maeneo mengine yanayozunguka mradi Wilayani Missenyi.

Mhandisi Msenyele alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba. “Ni vyema Mkandarasi ukatambua suala la muda, hakikisha mradi unakamilika kwa wakati, wananchi wanausubiri huu mradi kama walivyoahidiwa,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.

Mara baada ya kusaini mkataba, Mhandisi Msenyele alimtaka Mkandarasi kuelekea eneo la mradi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kuanza ujenzi hasa ikizingatiwa kwamba ujenzi wa mradi ulipaswa kuwa umekwisha anza.

“Hakuna sababu ya kuchelewa, mipango yote ipo tayari na kwakuwa tumekwisha saini mkataba ni vyema ukafika eneo la mradi na kujipanga ukiwa huko huko, suala la muhimu kwa sasa ni nyinyi kufika eneo la mradi,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.

Kwa upande wake Mhandisi Mradi wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi He Jun alimhakikishia Mhandisi Msenyele kwamba watahakikisha wanakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba.

Ujenzi wa mradi wa maji Kyaka Bunazi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai 11, 2019.


Ad

Unaweza kuangalia pia

Askofu Dkt Maasa OleGabriel RAIS SAMIA ANATEKELEZA MAAGIZO YA MUNGU YA KUITUNZA BUSTANI YA EDENI

Askofu Dkt. Maasa OleGabriel Katibu Mkuu Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania na Askofu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *