NAIBU WAZIRI NISHATI AZINDUA MRADI WA UMEME JUA NANJIRINJI

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye ushungi-kulia), akizungumza na baadhi ya viongozi na wawakilishi wa wananchi wa Kata ya Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi, alipokuwa katika ziara ya kazi ambapo alizindua rasmi mradi wa umeme jua, Mei 17, 2020.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezindua rasmi mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika vijiji vya Kata ya Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Akizungumza na viongozi wa eneo hilo akiwemo Mkuu wa Wilaya, Diwani na viongozi wa vijiji husika, muda mfupi kabla ya kufanya uzinduzi, Mei 17, 2020, Naibu Waziri alieleza kuwa mradi huo unalenga kuwapatia huduma ya umeme wananchi wakati serikali ikijiandaa kupeleka umeme wa uhakika kupitia mradi wa umeme vijijini.

Ad

“Tunashukuru Bunge kwa kupitisha bajeti ya Wizara yetu kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambayo pamoja na mambo mengine, imejikita katika upelekaji umeme vijijini. Nafurahi kuwajulisha kuwa vijiji vya Nanjirinji ni miongoni mwa vitakavyopelekewa umeme ndani ya kipindi husika,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri alieleza kuwa mradi huo ambao pia unatekelezwa Kilwa kisiwani ni mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya umeme mkubwa, vikiwemo visiwa, wanafikishiwa pia huduma ya umeme ili waweze kunufaika sawa na wananchi wa maeneo mengine.

Aliwataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ndiyo wafadhili wa miradi ya aina hiyo kote nchini, kujenga utaratibu wa kutembelea miradi hiyo ili kujiridhisha endapo fedha zilizotolewa na Wadau wa Maendeleo katika kutekeleza miradi hiyo zinatumika kwa tija.

Kwa mantiki hiyo, aliutaka Wakala huo kuanzisha kitengo cha tathmini na ufuatiliaji, ambacho kitashughulikia masuala hayo katika miradi yote ya umeme jadidifu.

Halikadhalika, alitoa maelekezo hayo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“TANESCO ninyi ndiyo mnahusika na uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo mnawajibika pia kufuatilia miradi hii na kufanya tathmini badala ya kuwaacha wananchi wakiwa hawana pa kukimbilia kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.”

Alisema, katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini kukagua miradi ya aina hiyo, amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuwa miradi hiyo haina mfuatiliaji badala yake anaachwa mkandarasi pekee pasipo usimamizi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitumia fursa hiyo kuwaeleza viongozi hao kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeanza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Likong’o mkoani humo, ambao wamepisha mradi wa kuchakata gesi.

Alisema jumla ya shilingi bilioni tano zimetolewa na kwamba mazungumzo yanaendelea baina ya serikali na wawekezaji kuhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachochochea uchumi wa Mkoa wa Lindi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS SAMIA ATEMBELEA RUKWA.. AANGAZIA AFYA, ELIMU, KILIMO NA MIUNDOMBINU KWA MIRADI YA MAENDELEO.

Katika ziara ya Rais Samia siku ya leo iliangazia kwenye sekta ya Afya, Elimu, Kilimo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *