Na Zuena Msuya Geita
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaambia wanakijiji ambao umeme ushafika katika maeneo yao walipie gharama za kuwashiwa umeme ili kufahamu idadi ya wateja, nguzo zisambazwe na kuunganishwa kulingana na wateja waliopo kwa wakati husika.
Dkt. Kalemani alisema hayo wakati akiwasha umeme katika Kijiji cha Rusungwa Kata ya Nyamirembe, Bugwego Kata ya Bwongera Wilayani Chato na Kijiji cha Businda Wilayani Bukombe mkoani Geita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Dkt. Kalemani alisema kuwa vijiji vingi tayari vimefikiwa na umeme katika maeneo machache hivyo wananchi wanatakiwa kulipia gharama za kuwashiwa umeme ili ifahamike idadi ya wateja waliopo na kupelekewa nguzo za kusambazwa kwa wateja waliopo na wawashiwe umeme.

Pia alieleza kuwa kitendo cha wanakijiji kuacha kulipia gharama za kuuwashiwa umeme wakisubiri kuona nguzo zimesambaa katika maeneo yao, hali ya kuwa tayari umeme umeshafika katika vijiji vyao, kunachelewesha kasi ya kuwawashia umeme wanakijiji katika nyumba zao kwa kuwa mamlaka husika zinasambaza nguzo kulingana na wateja waliopo eneo husika kwa wakati husika, hivyo wananchi wachangamkie fursa na kulipia gharama ya shilingi 27,000 tu.
Vilevile alisema kuwa wanakijiji hao hawapaswi kuhoji kuhusu nguzo kufika katika maeneo yao kwakuwa hilo si jukumu lao, ila wanachotakiwa kufanya ni kulipia gharama za kuwashiwa umeme tu, na baada ya kulipia gharama ndipo wahoji endapo hawajawashiwa umeme.