MUDA WA KUKAMILISHA MIRADI HAUJABADILIKA – WAZIRI KALEMANI

Veronica Simba na Zuena Msuya – Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza na kujadiliana maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa nchini kote.

Ad

Kikao hicho kilichofanyika, Mei 21, 2020 jijini Dodoma kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo pamoja na Wajumbe wa Bodi hiyo.

Wengine ni Kaimu Kamishna wa Nishati Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Amos Maganga na Menejimenti yake, Mameneja wa TANESCO wa Kanda pamoja na Wasimamizi wa Mradi husika kutoka Wizarani.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (mstari wa mbele), wakishiriki kikao cha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo.

Akifungua kikao husika, Dkt Kalemani amewapongeza Wakandarasi hao kutokana na kazi wanayoifanya ya kusambaza umeme vijijini lakini amebainisha msimamo wa Wizara kuwa haitarajii kuongeza muda wa kukamilisha kazi husika, hivyo amewataka kuongeza bidii na ubunifu ili waweze kukamilisha kazi ifikapo Juni 30, mwaka huu kama ilivyoainishwa katika Mkataba.

“Pamoja na kwamba wengi wenu mnafanya kazi nzuri lakini wapo wachache ambao wanasuasua. Ninawataka mjipime kutokana na utendaji wenu kama mtastahili kuendelea na kazi nyingine zitakazofuata,” ameasa Waziri.

Akifafanua zaidi, amesema Wizara kamwe haitaingia mikataba mipya ya kazi na wakandarasi wababaishaji huku akisisitiza kuwa ni wale tu wanaofanya vizuri katika miradi ya sasa ndiyo watakuwa na nafasi ya kupewa kazi nyingine.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said (wa pili kushoto) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (hawapo pichani), wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini REA, Wakili Julius Kalolo.

Katika hatua nyingine, Waziri amewataka wakandarasi hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma hivyo amewataka kufanya kazi kwa weledi na uzalendo huku wakizingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwani ndivyo watumishi wa umma wanavyopaswa kuwa.

Amefafanua kuwa, mtumishi wa umma ni yeyote aliyeajiriwa au kuingia mkataba na Serikali kufanya kazi fulani na ataendelea kuwa na sifa hiyo hadi pale mkataba wake unapokoma.

Aidha, Waziri ametoa pongezi za pekee kwa wakandarasi ambao hadi sasa wamekamilisha kazi kwa asilimia nyingi huku wakiwa na uelekeo wa kukamilisha kazi husika muda mfupi kutoka hivi sasa.

Wakandarasi hao wametajwa kuwa ni Kampuni za Steg International Ltd anayetekeleza Mradi katika mikoa ya Mbeya na Songwe, Sengerema Engineering Group Ltd (Iringa), Derm Electrics (T) Ltd  (Tanga) na Nakuroi Investment Co. Ltd (Rukwa).

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka akizungumza na wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (hawapo pichani), wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na Wakandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 21, 2020 kujadili maendeleo ya Mradi huo.

Vilevile, Waziri ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa REA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia miradi husika. Pia, ameipongeza Menejimenti ya Wakala huo na watumishi wake wote huku akiipambanua Taasisi hiyo kwamba imetengeneza historia Tanzania.

“Tanzania sasa inasifika kwa kazi nzuri ya usambazaji umeme vijijini. Hilo limewezekana kwa uchapakazi wenu. Hongereni sana.”

Sambamba na REA, Waziri pia ameipongeza TANESCO, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa utendaji wao mahiri ambao ameeleza umewezesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Naye Katibu Mkuu amewaasa wakandarasi kujenga mahusiano mazuri na viongozi pamoja na wananchi wote katika maeneo wanakotekeleza miradi, ili iwasaidie kupata ushirikiano katika utekelezaji wa kazi zao.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA MRADI WA MAJI SAME MWANGA KOROGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji Maji wa Same – Mwanga – Korogwe wakati alipotembelea chanzo cha mradi huo eneo la la Nyumba yaMungu Wilaya ya Mwanga wakati akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024. Makamu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *