BODI YA UTALII TANZANIA: TUPO TAYARI KUANZA KUPOKEA WATALII

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema ipo tayari kuanza kupokea watalii wakati wowote kuanzia sasa kufuatia hatua ya Serikali kuruhusu kuendelea kwa shughuli za utalii nchini hatua iliyotokana na kupungua kwa kasi ya mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (CORONA) duniani.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Saalam na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo wakati wa mkutano wake na  Waandishi wa Vyombo vya Habari kuelezea mikakati endelevu ya TTB katika kutangaza shughuli za utalii nchini.

Ad

Jaji Mihayo alisema kufuatia kikao baina ya wadau wa utalii na Serikali kilichofanyika hivi karibuni Jijini Arusha, Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa mwongozo mahsusi wa namna ya uendeshaji wa shughuli za utalii nchini na unaotarajiwa kutafsiriwa kwa lugha mbalimbali na kusambazwa katika masoko ya utalii sehemu mbalimbali duniani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani Jijini Dar es Salaam, kuhusu kurejeshwa kwa huduma za utalii nchini, kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Bi. Devota Madachi.

‘Bodi ya Utalii Tanzania imeshiriki kikamilifu kwenye kikao hicho  na mwongozo uliotolewa utahakikisha kuwa Watanzania wanakua salama na watalii pia wanatalii kwenye vivutio vilivyo na usalama na kuhakikisha kuwa shughuli za kutangaza utalii hazisimami kutokana na janga la corona duniani’’ alisema Jaji Mihayo.

Kwa mujibu wa Jaji Mihayo alisema TTB pia imepanga kufanya kufanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya kupokelea na kulaza watalii ili kujiridhisha kuwa maeneo hayo yana huduma mbalimbali za dharura kulingana na mwongozo ulitolewa na Serikali ili kuhakikisha kuwa utalii wa Tanzania unaendelea kuwa salama.

Aidha Jaji Mihayo alisema mara baada ya zoezi hilo kukamilika TTB itaanza kufanya mazungumzo na Ofisi za Ubalozi wa Tanzania na Balozi za masoko ya utalii wa Tanzania zilizopo nchini ili kuwahakikishia  hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusiana na udhibiti wa mlipuko wa virusi vya COVID-19 kabla ya kuruhusu watalii kuanza kuwasili nchini.

Akifafanua zaidi Jaji Mihayo alisema TTB kwa kushirikiana na sekta binafsi imetengeneza filamu mbalimbali za vivutio vya utalii nchini ili kuhakikisha kuwa shughuli za kutangaza utalii hazisimami kutokana na janga la CORONA, ikiwemo kampuni ya Great Migration Camp walioanzisha kipindi cha ‘Serengeti Live Show’ kinachorushwa katika mitandao yote ya kijamii ya TTB na Serengeti Live YouTube Channel.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii (TTB), Bi. Devota Madachi akiandika swali kutoka kwa waandishi wa habari katika Mkutano wa Waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo pichani Jijini Dar es Salaam, kuhusu kurejeshwa kwa huduma za utalii nchini.

‘Nitoe wito kwa wafanyabiashara wa sekta ya utalii, kujitolea kwa hali na mali kutangza filamu hizi ambazo zimesaidia kutangaza utalii wa Tanzania duniani, na televisheni zetu za ndani zinaweza kuzipata filamu hizi bure bila malipo hapa TTB ili mkaziongeze kwenye ratiba za vipindi vyenu kama sehemu ya kutoa elimu’ alisema Jaji Mihayo.

Kwa upande Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi alisema mwishoni mwa mwezi huu, ndege ya kwanza inatarajia kutua nchini ikiwa na watalii ambapo hadi sasa tayari wadau wote wa utalii wamekamilisha miongozo mbalimbali inayotakiwa kufuatwa ili kuwakinga watalii na maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Aidha Mdachi alisema Serikali pia i imefanya mawasiliano na Ofisi za Ubalozi wa Tanzania katika nchi za Israel, China na Malaysia ili kuhamasisha  makundi makubwa ya watalii wa nchi hizo waliopanga kuja Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu kufufua mipango yao ya safari ya kutembelea vivutio vya utalii nchini.  

Ad

Unaweza kuangalia pia

Uzinduzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya UCSAF Dodoma: Kuimarisha Mawasiliano Vijijini

25 Aprili 2024, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *