WAKULIMA IRINGA NA MBEYA KUNUFAIKA NA MRADI WA BARABARA ZA LAMI

Na. Geofrey A. Kazaula

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA unaendelea na mpango wake wa kujenga barabara za lami kupitia mradi wa Agri-Conect ili kuhakikisha wakulima wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka mashambani hadi viwandani na sokoni.

Ad

Mradi huo wa Agri–Conect unaotekelezwa katika Mikoa ya Mbeya na Iringa umepokelewa kwa shangwe na wananchi wa maeneo hayo nakueleza kuwa wanaona kama ndoto kujengewa barabara za lami na kwamba kupitia barabara hizo watajikomboa kiuchumi.

Barabara hizo za lami kuelekea mashambani zitakuwa na urefu wa Kilometa 87.6 na barabara zitakazojengwa ni pamoja na Kidabaga – Boma lang’ombe yenye urefu wa kilometa 18.3 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Barabara ya Sawala -Mkonge – Luhunga yenye urefu wa kilometa 18.0 na Luhunga – Lyegeya  yenye urefu wa kilometa 12.3  katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya barabara zitakazojengwa ni Pamoja na Inyara – Simambwe yenye urefu wa kilometa 16.7 na Lupeta – Wimba – Izumbwe  yenye urefu wa kilometa 10.1 ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Barabara zitakazojengwa ni Pamoja na Masebe Dispensary – Mpuguso TTC – Bugoba – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 5.0 na Masebe – Bugoba – Lutete yenye urefu wa kilometa 7.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Bw. Peter Francis ambaye ni Mkazi wa Kata ya Mkonge katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, ameeleza kuwa baada ya kuiona dhamira ya Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini ya kuwajengea barabara ya lami walihamasika sana na kuamua kubomoa nyumba zao bila kudai fidia ili kupisha ujenzi huo.

‘‘Tumehamasika sana na kama unavyoona, tumebomoa nyumba zetu bila kudai fidia ili kupisha ujenzi wa barabara ya lami kwa sababu tuna amini kuwa barabara hii ni mkombozi kwetu kwani sasa mazao yetu yatasafirishwa kwa urahisi”, alisema Peter.

Naye, Bw. Richard Mandindi ambaye ni Mkazi wa Kata ya Kisondera katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ameipongeza  Serikali ya awamu ya tano kwa kuanza kutatua changamoto  ya muda mrefu baada ya ujenzi wa barabara ya lami katika Kata hiyo kuanza.

‘‘Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuona sisi wananchi wa Vijijini, tulikuwa hatuwezi kusafirisha mazao yetu kama ndizi, chai na kahawa lakini sasa barabara inajengwa na tunaona kama ndoto kwasababu hatukutarajia kitu kama hiki  kufanyika kwetu”, alisema  Richard.

Kwaupande wake Mratibu wa miradi inayofadhiliwa na umoja wa Ulaya – EU kupitia Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini – TARURA Mhandisi Daudi Sweke ameeleza kuwa miradi hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kwamba imejikita katika maeneo yanayozalisha sana ili kuwasaidia wakulima.

‘‘Tafiti zilijikita katika maeneo yanayozalisha sana huku yakiwa na changamoto ya barabara, lakini pia hapa ni mwanzo kwani tutaendelea kuboresha mazingira ya wakulima katika maeneo mbalimbali kwa mwaka wa fedha ujao’.

Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Gerald Matindi ameeleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa barabara za lami utasaidia sana wananchi kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi barabara kuu ili kupelekwa sokoni.

Miradi hiyo ya ujenzi wa barabara za lami kuelekea mashambani kwa mikoa ya Mbeya na Iringa tayari imeanza kutekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA.

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tusikubali Kuwa Tarumbeta za Watu Wasio Tutakia Mema”

“Tusikubali kuwa tarumbeta za Watu wasio tutakia mema, Maadili Yetu Mazuri Ya Kitanzania Lazima Tuyatunze, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *