RAIS MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI WA TATU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Oktoba, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 3 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Mhe. David William Cancar (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Uingereza hapa nchini), Mhe. Muhammad Saleem (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Pakistan hapa nchini) na Mhe. Didier Chassot (aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Uswisi hapa nchini).

Ad
Mhe.Rais John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi David William Conca Balozi wa Uingereza nchini mara baada ya kupokea hati ya utambulisho

Mabalozi hao wameahidi kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zao ikiwemo kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini, kuvitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika nchi zao, kununua bidhaa za Tanzania kama mazao ya kilimo na madini na kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara wa nchi zao ili kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi hizo.

Mhe.Rais John Pombe Magufuli akiwa na Balozi David William Conca Balozi wa Uingereza nchini mara baada ya kupokea hati ya utambulisho

Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. David William Cancar amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake mzuri ambapo Tanzania kwa kufanikiwa kuingia katika uchumi wa nchi za kipato cha kati, kusambaza umeme kwa kasi kubwa, kutoa elimu bure, kujenga miundombinu hasa barabara, kupambana na rushwa na amekiri kuwa inauona utekelezaji wa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

Muhammad Saleem Balozi wa Pakistan nchini akisaini baada ya kuwasilisha hati ya utambulisho kwa Rais Dkt. John Magufuli Ikulu Dar es salaam leo.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mhe. Rais Magufuli, tunatazamia kukuza zaidi uhusiano wa Uingereza na Tanzania hasa katika biashara, kwa sasa biashara yetu ni takribani shilingi Bilioni 390 kwa mwaka na pia tunachangia takribani shilingi Bilioni 800 kwa mwaka katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapa Tanzania. Matarajio yangu ni kuwa tutaongeza Zaidi” – amesema Mhe. David William Cancar alipozungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho.

Rais. Dkt.John Pombe Magufuli,katika picha ya pamoja na Mhe. Muhammad Saleem Balozi wa Pakistan nchini Ikulu jijini Dar es salaam leo.

Balozi wa Pakistan hapa nchini, Mhe. Muhammad Saleem ameelezea kufurahishwa kwake na maendeleo ya Tanzania na ameahidi kuwaunganisha wafanyabiashara wa Pakistan na Tanzania ili kupanua zaidi uwigo wa biashara na kuongeza ununuzi wa bidhaa za Tanzania hasa kahawa, pamba, korosho na chai.

Balozi wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Didier Chassot amesema Uswisi inao mkakati wa miaka 4 ambapo atahakikisha utekelezaji wa mkakati huo unaleta manufaa yaliyotarajiwa hasa kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya kuzalisha ajira, kuongeza kipato, kuboresha huduma za afya, na utawala bora.

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na DidierChassot Balozi wa uswizi mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikulu Dar es salaam leo

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wowote utakaohitajika katika utelekezaji wa majukumu yao.

Mhe. Rais Magufuli amewataka kutoa kipaumbele katika uchumi kwa kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini ambapo watanufaika na uwepo wa malighafi, soko la uhakika na mazingira bora ya uwekezaji.

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli leo amepokea Hati za utambulisho wa Mabalozi wa Uingereza.Uswizi na Pakistan, Pichani mhe.DidierChassot Balozi wa uswizi akiwa katika picha mbalimbali wakati wa kuwasilisha hati hizo kwa mhe .Rais Dkt.John Pombe Magufuli ikulu Dar es salaam leo

Pia, Mhe. Rais Magufuli amewaalika viongozi wakuu wa nchi hizo kutembelea Tanzania.

Hafla ya kupokea hati za utambulisho za Mabalozi hao zimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *