RAIS AMEWAAMINI WAZALENDO KUTEKELEZA JNHPP – NAIBU KATIBU MKUU MASANJA

Veronica Simba – Rufiji

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuwaamini wazalendo katika kusimamia utekelezwaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Ad

Alitoa pongezi hizo Oktoba 3, 2020 wakati akizungumza na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), waliotembelea Mradi huo unaotekelezwa wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, ili kujionea maendeleo yake.

Mhandisi Masanja alisema kuwa hatua ya Mheshimiwa Rais kuwaamini wataalamu wazalendo kusimamia usanifu wa awali, hatua za manunuzi na hata usimamizi wa utekelezaji wa mradi wenyewe, pasipo kushirikisha wataalamu wa kigeni ni ushahidi kuwa Tanzania ina hazina ya wataalamu mahiri.

Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ukiendelea katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji, mkoani Pwani. Taswira hii ilichukuliwa Oktoba 03, 2020 wakati Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (hawapo pichani), walipozuru Mradi huo ili kujionea maendeleo yake.

“Kupitia Mradi huu, tumeudhihirishia ulimwengu kuwa Tanzania ina wataalamu mahiri na kwamba sisi wenyewe tunaweza kusimamia miradi yetu.”

Akifafanua, alieleza kuwa Serikali iliamua kuwatumia wataalamu kutoka TANROADS (TANROADS Engineering Consulting Unit – TECU) kama Mshauri Mwelekezi wa Mradi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kama wawakilishi wa Serikali katika kusimamia Mradi husika ili kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza kazi zote kwa mujibu wa Mkataba.

Aidha, aliongeza kuwa, jambo la kujivunia zaidi ni kuwa Mradi huo unatekelezwa na fedha za Serikali kwa asilimia 100, hivyo akawataka Watanzania kujivunia Mradi huo kwani nchi inaumiliki kikamilifu.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakikagua miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani. Ujumbe huo ulitembelea Mradi husika, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.

Awali, akitoa wasilisho la Mradi kwa Ujumbe husika, Mhandisi Mkazi wa Mradi huo, Mushubila Kamuhabwa, alisema kuwa katika hatua ya ujenzi inayoendelea sasa, Mradi umewezesha uzalendo na mshikamano wa hali ya juu kwa vijana wa kitanzania wanaofanya kazi za ujenzi.

“Ni kama wakati ule vijana walipokuwa wakishiriki mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Utawakuta vijana hawa wakiimba nyimbo za kizalendo wakati wanafanya kazi na pia wakishirikiana kwa kila jambo, hali inayoonesha wazi wanajisikia fahari kuwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi huu.”

Vilevile, Mhandisi Kamuhabwa alibainisha kuwa miongoni mwa waajiriwa 5,500 wa Mradi waliopo sasa, Watanzania ni 4,900 ambao ni takribani asilimia 90 ya waajiriwa wote, jambo ambalo linadhihirisha dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele katika kila sekta ya Mradi huo.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakikagua miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani. Ujumbe huo ulitembelea Mradi husika, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.

Aidha, alibainisha faida nyingine ambazo zimekwishaanza kupatikana katika hatua hii ya awali ya utekelezaji wa Mradi kuwa ni pamoja na matumizi ya rasilimali za ndani ya nchi kama vile nondo, saruji, vyakula, ulinzi na nyinginezo.

Kuhusu faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa Mradi, alisema pamoja na kuzalisha umeme mwingi utakaokuwa na bei nafuu, Mradi huo pia utakuza sekta za utalii, kilimo, uvuvi wa samaki pamoja na kuboresha mazingira kutokana na kupungua kwa ukataji miti kwa matumizi ya mkaa na kuni.

Alitaja faida nyingine kuwa ni kudhibiti mafuriko kwa kudhibiti maji ya Mto Rufiji ambayo awali yalikuwa yakileta majanga ya kuua watu na kuharibu mali zao.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakikagua miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani. Ujumbe huo ulitembelea Mradi husika, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Mwenyekiti wake, Wakili Julius Kalolo alipongeza kazi inayofanyika ambapo alisema yeyé na wenzake wameridhishwa na kasi pamoja na viwango katika utekelezaji huo wa Mradi.

Aliongeza kuwa pindi Mradi huo utakapokamilika utaongeza nguvu zaidi kwa Wakala huo kufikisha umeme kwa kila kaya, ikizingatiwa kuwa tayari taasisi hiyo imeanza utekelezaji wa kupeleka umeme katika kila kitongoji nchini.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakikagua miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani. Ujumbe huo ulitembelea Mradi husika, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.

Naye Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma alisema kuwa Wizara iliona umuhimu wa kuandaa ziara hiyo kwa ajili ya Wajumbe wa Menejimenti yake, ili kuwawezesha kujionea kwa macho kinachofanyika ikizingatiwa kuwa ndiyo Wizara Mama inayohusika na Mradi huo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *