Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itawekeza kwenye michezo katika kuibua, kulea na kuendeleza vipaji vya vijana.
Rais Dkt. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.
Rais Dkt. Hussein aliongeza kuwa azma ya Serikali ni kuona Timu ya Taifa ya Zanzibar inakwenda mbali katika kushiriki michuano ya Afrika ili kutumia vizuri fursa ya uanachama katika Shirikisho la Michezo la Kimataifa (CAF)
Aidha, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alieleza kwamba eneo jengine ambalo litafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Nane ni kushughulikia Sanaa, burudani pamoja na michezo kwani mambo hayo matatu yana nafasi ya kipekee katika kuwaunganisha Wazanzibari, kuwatambulisha Wazanzibari duniani na kukuza uchumi na ajira.
Aliongeza kuwa Muziki wa Taarab, muziki wa kizazi kipya na Sanaa ya filamu kupitia matamasha ya ZIFF na ‘Sauti ya Busara’ yameitangaza sana Zanzibar na kuwa na mchango wa kipekee hivyo, aliahidi kuyalea na kuyakuza matamasha hayo na mengine ili kutangaza hazina ya utamaduni na ustaarabu wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii, kipato pamoja na ajira.