MKANDARASI ATAKIWA KUMALIZA UJENZI WA BARABARA ZA MJI WA SERIKALI IFIKAPO JULAI 2021

Na. Bebi Kapenya

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amemuagiza Mkandarasi Kampuni ya China Heinan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) anayetekeleza Mradi wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami zenye urefu wa Km 51.2 katika Mji wa Serikali Mtumba kukamilisha kazi kwa muda na katika viwango vinavyotakiwa ifikapo tarehe 31 Julai 2021.

Ad

Mhandisi Seff ametoa agizo hilo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa barabara hizo zinazoendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na kubaini kuwa kuna ucheleweshaji wa muda uliowekwa kwa asilimia mbili (2%) kwani ujenzi umefikia asilimia 54 ambapo kwa mujibu wa ratiba ilitakiwa kufikia asilimia 56.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff (wa pili kutoka kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi alipofanya ukaguzi wa Mradi wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami zenye urefu wa Km 51.2 katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

“Kimsingi suala la kuongezewa muda halipo kabisa kwenye huu ucheleweshaji wa asilimia 2, hakikisheni mnaongeza nguvu ya kufanya kazi na kuhakikisha mnamaliza kwa wakati kulingana na mkataba na ifahamike wazi kuwa kushindwa kukamilisha kwa wakati itapelkea kupewa adhabu kwa kukatwa kiasi cha fedha kama ilivyoainishwa kwenye mkataba”, alisema Mhandisi Seff.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hizo unaogharimu Shilingi Bilioni 88.1 unahusisha ujenzi wa barabara za njia nne zenye urefu wa Km 11.2, ujenzi wa njia mbili zenye urefu wa Km 28.8, ujenzi wa kalavati, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, ujenzi wa barabara za waenda kwa miguu pamoja na taa za barabarani.

Aidha, amemtaka Mkandarasi huyo kuongeza kasi katika uzalishaji wa “U drains” zinazotumika kwa ajili ya mifereji na kwamba badala ya kutumia njia moja tu wanatakiwa kutumia njia zote mbili ili kuendana na muda.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff (wa tatu kutoka kushoto) akipata maelezo kwenye michoro inayotumika katika Mradi wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami zenye urefu wa Km 51.2 katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Pia, Mkandarasi huyo ameagizwa kuangalia suala la usalama na jinsi ya kuongoza magari kwasababu njia hizo bado zinatumika kwenda kwenye maofisi mbalimbali ya Serikali yaliyopo Mtumba.

“Kimsingi hatua ambazo zimewekwa katika suala zima la usalama katika kuwaelekeza madereva hazitoshi kabisa hivyo, nawaelekeza muweke vibao vya kutosha na alama za kutosha ili kuwaelekeza madereva kufika kwenye ofisi mbalimbali za Serikali”, alisema Mtendaji Mkuu huyo.

Mradi wa ujenzi wa Barabara za Mji wa Serikali Mtumba unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unatekelezwa na Mkandarasi China Heinan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) kwa muda wa miezi 18 ambapo unatarajia kukamilika ifikapo tarehe 31 Julai 2021.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mama Mzazi wa Mama Janeth Magufuli (Juliana Stephano Kidaso) katika eneo la Kigongo Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *