WATUMISHI WA TANESCO WATAKIWA KUJIANDAA KUIJENGA TANESCO MPYA

Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam.

Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamewatakiwa kuwa tayari kupokea mabadiliko, kufanya kazi kwa bidii na weledi na kutoa ushirikiano mzuri kwa uongozi wa TANESCO na bodi mpya iliyoteuliwa ili kulijenga upya Shirika la TANESCO na  kuliwezesha kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.

Ad

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba tarehe 26 Septemba, 2021 alipokuwa anazungumza na watumishi wa TANESCO kwenye mkutano wake na Mameneja wa TANESCO uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam.

Waziri Makamba amewaambia watumishi wa TANESCO, kuanzia sasa, hakutakuwa na uonevu kabisa kwenye Shirika la TANESCO na kuwa, wafanyakazi wajiweke tayari kufanya kazi kwa ushirikiano, bidii na maarifa ili kuongeza utendaji wenye tija.

Amesema, uteuzi uliofanywa wa viongozi wa juu wa Menejimenti ya TANESCO na Bodi, unatoa taswira na ishara namna ambavyo Serikali inataka shirika la TANESCO liongozwe.

Aidha, Waziri Makamba ameeleza kuwa, mkutano huo umelenga kufahamiana na kuutambulisha uongozi mpya kwa watumishi hao wa TANESCO na kuwa, uteuzi na utenguzi uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na ule uliofanywa na yeye Waziri wa Nishati, unamaanisha kuwa, Serikali inataka mapinduzi makubwa katika sekta ya umeme.

“Tunataka shirika letu liendeshwe kwa ufanisi, kibiashara, liwe shirika linalowajali watumishi wake, linalochangia kwenye maendeleo na ukuaji uchumi hapa nchini na linaloheshimika zaidi Afrika Mashariki. Tumewaletea uongozi mpya, bodi mpya na sasa tunaanza safari yenye mwelekeo mpya.” Alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba aliongeza kuwa, Serikali  haitavumilia wizi, dhuluma wala hujuma na inatarajia kiwango cha juu sana cha uadilifu na uchapa kazi na kuwa, hiyo ni ahadi inayopeana kati ya viongozi na Serikali.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni kwa uongozi wa TANESCO, Waziri Makamba amesema, ni uamuzi mgumu sana kumuondoa mtu kazini hasa  mtu mwenye nafasi kubwa kama Mkurugenzi Mkuu, mtu wa manunuzi, mtu wa sheria, lakini ni uamuzi ambao ni wa lazima ili kufikia malengo.

“Na uamuzi huo tumeuchukua kwa sababu tunataka mambo yaende. Hawa walioondolewa wamefanya kazi mpaka walipotufikisha, na haina doa kwamba ni watu ambao ni wa ovyo ila tunataka mwelekeo mpya. Na tunahitaji timu mpya ambayo itatupeleka kule tunarajia. Alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba amewaambia watumishi hao wa TANESCO kuwa, Mwenendo mpya ni kuwa, atakayefanya kazi vizuri, ataonekana na atatunukiwa. “Tunaamini kwamba mabadiliko yaliyofanyika na mwelekeo mpya mmeupokea na mtautekeleza” alisema Waziri Makamba.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema, bodi iliyoteuliwa ni muhimu sana kwa maendeleo ya shirika la TANESCO na kuwa Wizara ya Nishati inaitegemea sana bodi hiyo katika kutoa ushauri utakaoiwezesha TANESCO kufikia malengo yanayotarajiwa.  

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Bw. Maharage Chande amewaambia watumishi hao wa TANESCO kuwa, malipo yatatokana na utendaji. Kama mtumishi anafanya kazi vizuri apewe aneemeke na mtumishi asiyefanya kazi vizuri afundishwe, na iwapo baada ya kufundishwa mtumishi bado hafanyi vizuri basi mtumishi huyo atakuwa hafai.

Bw. Chande amesema, maamuzi magumu hayawezi kufanikiwa bila kuwa na ushirikiano wa pamoja baina ya watumishi na viongozi na kuwataka watumishi wa TANESCO kwa pamoja washirikiane kuyatafuta yaliyo mazuri na pia washirikiane kuyakataa mabaya.

“Malipo kutokana na utendaji, ushirikishwaji wa wafanyakazi, motisha kwa wafanyakazi, uendelezaji wa watumishi kitaaluma, mpango mzuri wa kurithisha vyeo watumishi, ndiyo yatakayopewa uzito wa juu na yatafanyika kwa haraka sana.” Amesema Chande.

Aidha, Bw. Chande amewatahadharisha watumishi hao wa TANESCO kuwa, wakati wa kuanza safari ya kuijenga TANESCO mpya, watakutana na changamoto na kuwataka wawe jasiri katika kusonga mbele.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo wa TANESCO amesema, mara baada ya kikao hicho, atakutana na Mameneja hao wa TANESCO ili kutoa dira na mwelekeo wa shirika wenye lengo la kuifanya TANESCO kuwa shirika bora si tu kwa Afrika Mashariki bali katika bara la Afrika.

Naye mwenyekiti wa bodi ya TANESCO Bw. Omari Issa amesema, mabadiliko yanayotarajiwa kwa TANESCO yatafanywa na watumishi wa TANESCO wenyewe. Na kuwa, kipaumbele cha kwanza ni Rasilimali watu na kusisitiza kuwa kila mtumishi wa TANESCO awe tayari kubadilika ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na Serikali kwa Shirika la TANESCO.

Amewaomba watumishi wa TANESCO waiunge mkono bodi ya TANESCO na kuyakubali mabadiliko ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Bw. Issa amemuomba Waziri wa Nishati kufikisha salaam zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuiongoza bodi ya TANESCO na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa na kwa kujituma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mameneja wa Kanda – TANESCO wamempongeza Waziri Makamba kwa uteuzi na kwa hotuba nzuri aliyoitoa kwa watumishi wa TANESCO yenye matumaini ya kuijenga kiupya TANESCO kwa lengo la kuongeza ufanisi na utendaji wenye tija.

Nae Meneja Mwandamizi wa Rasilimali watu Fransis Sangunaa, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa TANESCO, amesema, watumishi wa TANESCO watatoa ushirikiano mkubwa na wa kutosha ili kuyafikia malengo yale ambayo Serikali inatarajia kuyafikia kupitia shirika la TANESCO.

Akitoa neno la shukrani katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, amewapongeza viongozi walioteuliwa na kuwashukuru viongozi hao kwa kushiriki katika kikao hicho muhimu.

Vile vile kwa niaba ya watumishi wote wa Wizara ya Nishati, amemshukuru Waziri wa Nishati kwa muongozo alioutoa na kuahidi kuwa viongozi wa Wizara ya Nishati pamoja na watumishi, wako tayari kutoa ushirikiano ili kuwezesha mapinduzi ya Nishati kwa ajili ya maendeleo makubwa zaidi.

Mkutano huo, umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha.  Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba, Kamishna wa Petrol na Gesi, Michael Mjinja, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa na mameneja wa TANESCO nchini

Ad

Unaweza kuangalia pia

MWENDO KASI LEOTakwimu za Sasa za Utekelezaji wa Mradi wa Mwendo Kasi kwa Mwaka 2024

Mradi wa Mwendo Kasi (BRT) nchini Tanzania unaendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wake mwaka …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *