#MATAGA WIZARA YA MAJI; HADI SASA VITUO 123,888 VYA KUCHOTEA MAJI VIMEJENGWA KATIKA VIJIJI NCHINI!

 • Maji ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi. Tanzania inakadiriwa kuwa na rasilimali za maji juu ya ardhi zenye kilomita za ujazo 92.27 na chini ya ardhi kilomita za ujazo 38. Utunzaji na uendelezaji wa rasilimali hizo unasimamiwa na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na Sera, Sheria na Kanuni zake.
 • Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inaelekeza kuwapatia wananchi waishio vijijini maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji.

WAZIRI WA MAJI PROF MAKAME

 • Lengo ni kufikia asilimia 85 ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2020. Hadi sasa, miundombinu ya maji iliyojengwa ina jumla ya vituo vya kuchotea maji 123,888 ambavyo vina uwezo wa kuhudumia watu 30,972,000 sawa na asilimia 85.2 ya wananchi 36,344,509 waishio vijijini. Hata hivyo, kati ya hivyo, vituo 85,286 tu ndivyo vinavyofanya kazi na kutoa huduma kwa watu 21,321,500 sawa na asilimia 58.7 ya wananchi waishio vijijni wanaopata huduma ya majisafi na salama. Hali hiyo imechangiwa na changamoto ya mfumo uliopo wa usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji.
 • Kwakuliona hilo, Serikali kupitia bunge tukufu imeamua kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini – Rural Water Agency (RUWA) chombo ambacho kipo katika hatua za mwisho za kisheria kabla ya kuanza kutumika rasmi. Kupitia mifano mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu katika kuwahudumia na kuwanufaisha wananchi, RUWA inategemewa kuwa ni muarobaini wa tatizo kubwa la usimamizi wa miradi ya maji vijijini.
MRADI WA MAJI NANSIO UKEREWE MKOANI MWANZA
mradi wa maji Nansio Ukerewe Mkoani Mwanza.
 • Kumekuwa na changamoto kubwa katika kusimamia miradi ya maji vijijini kwa jumuiya za maji kushindwa kusimamia miradi kwa umakini jambo ambalo linapelekea miradi mingi kutokuwa endelevu na hatimaye kuisababishia serikali hasara kubwa.
 • Kwa upande mwingine, miradi mingi ya maji vijijini inaendeshwa kwa kutumia nishaji ya dizeli ambayo nayo imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji. Katika kuwapunguzia kuwapunguzia wananchi gharama za uendeshaji na matengenezo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kubadilisha mitambo inayotumia nishati hiyo ya dizeli.

MATAGA - 25

 • Kwa upande wa utoaji huduma ya majisafi na uondoaji majitaka maeneo ya mijini, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika miji mikuu ya mikoa ni wastani wa asilimia 78. Kiwango hicho kimeshuka ikilinganishwa na asilimia 86 ya mwaka 2016/2017 kutokana na kuongezeka kwa eneo la utoaji wa huduma baada ya upanuzi wa mipaka ya baadhi ya miji, kuanzishwa kwa miji mipya pamoja na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji. Katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji midogo na Miradi ya Kitaifa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ni wastani wa asilimia 60. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 75.
 • Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2015 – 2020) inaelekeza kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini kufikia asilimia 95 katika miji mikuu ya mikoa na Dar es Salaam; na asilimia 90 katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa. Azma ya Serikali ni kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya miji nchini.

MATAGA - 23

 • Katika kuhakikisha Serikali inatimiza kiwango hicho kama kilivyoainishwa kwenye ilani ya Chama tawala, ipo mikakati mbalimbali ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika ya dini na taasisi kwa pamoja wanajenga miradi mipya ya maji na kukarabati ya zamani ili kuwapatia wananchi wa Tanzania majisafi na salama.
 • Wakati alipokuwa akizindua mradi wa maji wa Ruvu Juu kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam, mji wa Mlandizi, Kibaha na maeneo yanayopitiwa na bomba; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipokea mkopo wa masharti nafuu kutoka seikali ya India wa (Dola za Marekani milioni 500) kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji nchini. Kupitia mkopo huo, awali Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo 17 nchini ikihusisha Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo, Miradi ya Maji ya Kitaifa pamoja na Zanzibar.

MATAGA - 24-01

 • Hata hivyo, baada ya kufanya tathmini upya na kushauriana na Benki ya Exim- India, ilionekana kuna uwezekano wa kuongeza miji mingine katika mradi huu bila kuongeza gharama. Hivyo, mradi huu sasa utatekelezwa katika miji 26; Muheza, HTM- Korogwe, Makonde, Kilwa Masoko, Wanging’ombe, Makambako, Njombe, Songea, Chunya, Rujewa, Mafinga, Manyoni, Sikonge, Singida, Kiomboi, Mpanda, Chemba, Urambo-Kaliua, Mugumu, Geita, Kayanga, Kasulu, Pangani, Ifakara, Engiri juu – Tarime na Zanzibar.
 • Utekelezaji wa miradi hiyo itafanywa kwa kanda 5 yaani; Kanda Na. 1: Muheza, HTM- Korogwe, Makonde, Pangani, Ifakara na Kilwa Masoko; Kanda Na. 2: Wanging’ombe, Makambako, Njombe, Songea, Chunya, Rujewa na Mafinga; Kanda Na. 3: Manyoni, Sikonge, Singida, Kiomboi, Mpanda, Chemba na Urambo – Kaliua; Kanda Na. 4: Mugumu – Mara, Geita, Kayanga, Engiri juu – Tarime na Kasulu; na Kanda Na. 5: kwa ajili ya uboreshaji huduma ya maji Zanzibar. Mkataba wa Kifedha kati ya Serikali ya Tanzania na India ulisainiwa tarehe 10 Mei, 2018 hatua ambayo iliruhusu utekelezaji wa mradi kuanza. Utekelezaji wa mradi upo katika hatua ya ununuzi.
 • Aidha, Serikali kwa kushiriana na Benki ya Dunia (WB) wamesaini Mkataba wa kifedha wa Dola za Marekani Milioni 350 takriban Tsh. Bilioni 800 kwa ajili ya kuendeleza programu endelevu ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini katika wilaya 86 zilizopo kwenye mikoa 17 ya Tanzania bara.
 • Programu hii itatekelezwa kwa kipindi cha miaka 6 kuanzia 2018 mpaka 2024, ambapo Wizara ya Maji ndiyo itakayoratibu kwa kusaidiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
 • Lengo la Programu hii ni kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama vijijini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la kufikia asilimia 85 ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama vijijini.
 • Programu italenga maeneo makubwa manne; Kukarabati miradi ya usambazaji maji vijijini; Kujenga miradi mipya ya usambazaji maji vijijini; Kupanua miundombinu ya usafi wa mazingira na Kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika utoaji huduma ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini.
 • Kupitia programu hii tunatarajia, Watu 2,500,000 watanufaika kwa huduma ya majisafi vijijini; Wananchi 4,000,000 watafikiwa na huduma ya majisafi na usafi wa mazingira; aidha, Vijiji 1,250 vitanufaika kwa huduma ya majisafi na salama.
 • Katika kuboresha huduma ya uondoaji majitaka jijini Dar es Salaam, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Korea Kusini, Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Benki ya Dunia inaendelea kuboresha huduma ya uondoaji wa majitaka pamoja na usafi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam.
 • Lengo ni kuongeza wastani wa upatikanaji wa huduma ya uondoaji majitaka kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2020. Katika kutimiza lengo hilo Serikali itajenga mitambo ya kusafisha majitaka katika maeneo ya Jangwani, Kurasini na Mbezi Beach pamoja na mtandao wa majitaka kutoka maeneo ya Ubungo, Kinondoni, Magomeni, Mwananyamala, Msasani, katikati ya Jiji na Ilala, Keko, Chang’ombe, Kurasini, Temeke na Uwanja wa Taifa, Mbezi Beach, Kawe na Kilongawima. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imetenga Shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DKT HASSAN ABBASI AKIONGEA NA WAANDISHI WA HABARI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *