SERIKALI YANEEMESHA WACHIMBA MADINI

 • Serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), imeendelea kunufaisha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuanzisha na kuboresha mifumo mbalimbali itakayosaidia kukuza sekta ya madini pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo.
 • Ujenzi wa Kituo cha Umahiri kilichopo katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kunatokana na Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inasisitiza sana juu ya uendelezaji wa sekta ya madini na hasa wachimbaji wadogo, ni hatua itakayosaidia kutatua changamoto za wachimbaji wadogo wa madini.
 • Mnamo Septemba 05, 2018 Kituo cha Umahiri cha Bariadi kilianza kujengwa na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT  na kusimamiwa na Kampuni ya Sky Actate Consultants, kilikamilika Oktoba 16 mwaka huu  na kugharimu  shilingi  bilioni 1.308, kitasaidia  kutoa  mafunzo na maarifa kwa wachimbaji wadogo kuhusu sera ya madini, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya kiutendaji katika shughuli za madini.

1-01

 • Aidha, kituo hicho kitasaidia kutoa elimu kuhusu ujasiriamali, utafutaji madini, uchimbaji madini, uchorongaji miamba, mazingira, afya na usalama migodini, pamoja na kutoa elimu juu ya mfumo wa kutathmini mashapo ya madini yaliyopo ili kufanya uchimbaji uwe na tija.
 • Akizungumza hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema ujenzi wa kituo hicho utajibu mahitaji ya mkoa katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kienyeji na kwenda kwenye uchimbaji wa kisasa.
 • “Wachimbaji wetu wadogo wamekuwa wakifanya shughuli zao kienyeji lakini uwepo wa kituo hiki utajibu mahitaji yao kwa sababu kitakuwa ni sehemu sahihi ya wao kupata elimu juu ya uchimbaji bora, pamoja na uwepo wa wataalam wa madini karibu na maeneo yao”, alisema Mtaka.
 •  “ Sisi kama mkoa tuna faida ya uwepo wa rasilimali madini tuna nikeli, shaba, dhahabu, cobalt, tuna chumvi katika wilaya ya Meatu lakini pia tuna madini ya ujenzi kama kokoto, mchanga na mengine, hivyo uwepo wa kituo cha umahiri kutasaidia wachimbaji kufanya kazi zao katika utaalamu ili uchimbaji ufanyike kwa ufanisi na uwe na tija”, alisisitiza Mtaka.
 • Naye, mchimbaji mdogo wa madini kutoka mkoa wa Simiyu, James Bundala, anasema kituo hicho cha umahiri ni kituo cha msaada katika kazi zao, na wanatarajia kitasaidia kuongeza tija na kukuza kipato kwa vile watafanya kazi kisasa zaidi.
 • “Imani yetu ni kuwa kituo hiki kitatusaidia kutatua migogoro ya uchimbaji madini inayojitokeza, pamoja na kupata elimu kuhusu uongezaji thamani madini na upatikanaji wa masoko, na haya yote yatatusaidia kufanya biashara yetu vizuri zaidi na kukuza vipato vyetu”, alisema Bundala.
 • Vile vile, kituo hicho kitasaidia katika usimamizi na uratibu wa shughuli mbalimbali zinazohusu madini, pamoja na kuwezesha wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi za maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao.
 • Katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, sekta ya madini imetekeleza hatua mbalimbali zenye lengo la kuimarisha sekta ya madini nchini kwa kuboresha maisha ya wachimbaji wadogo, sambamba na kuongeza pato la taifa.
 • Aidha, Serikali imefanikiwa kuifanya sekta ya madini kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa kuwekeza utaalam wa rasilimali watu, majengo, upimaji na utaalam mbalimbali wa kusaidia wachimbaji wadogo. Waziri wa Madini, Dotto Biteko, wakati alipokuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/20 alisema kuwa  mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa kwa mwaka 2018/19 umeendelea kuimarika na kufikia asilimia 5.07 mwaka 2018.
 • Mchango huo ulitokana na kuongezeka kwa uelewa kwa wadau wa sekta ya madini na kuwepo kwa uwazi katika shughuli zao, ukuaji wa sekta, kuimarisha usimamizi wa shughuli za madini kwa kudhibiti utoroshwaji, kuimarisha ukaguzi katika sehemu za uzalishaji na biashara ya madini, kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kupitia Marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123 yaliyofanyika mwaka 2017.
 • Aidha, Biteko amesema kuwa kuhusu uendelezaji wa uchimbaji mdogo wa madini, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa changamoto za sekta ya madini zinapatiwa ufumbuzi na hivyo kuwafanya wadau kufanya shughuli zao za uchimbaji na biashara ya madini katika mazingira ya kibiashara yanayovutia.
 • Mkakati mwingine  uliofanywa na Serikali  ili kuimarisha sekta ya madini  nchini ni pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kufanya mkutano na wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini  Januari 22 na 23 mwaka huu, kwa lengo la kuondoa changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta hiyo.
 • Katika mkutano huo, Serikali ilipokea kero na hoja mbalimbali zikiwemo, kupunguzwa kwa kodi na tozo zinazotozwa kwa wachimbaji wadogo wa madini, kufutwa kwa maeneo ya leseni za madini zisizoendelezwa na kuwekwa kwa maafisa madini kwenye maeneo ya machimbo ya madini.
 • Hoja nyingine katika mkutano huo zilikuwa, kudhibiti utoroshwaji wa madini, kuimarisha utunzaji wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji madini, ukosefu wa miundombinu, tozo na ada kulipwa kwa fedha za kigeni,  pamoja na kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio (withholding tax) asilimia 5 kwa wachimbaji wadogo. Hii inafanya jumla ya kodi zote zilizofutwa kufikia asilimia 23.
 • Ni dhahiri kuwa, katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya Awamu ya Tano inaimarisha sekta ya madini na kuneemesha wachimba madini kwa kuanzisha masoko ya madini na kujenga vituo vya mfano na umahiri ambavyo wachimbaji wadogo wanapata fursa ya kujifunza teknolojia na mbinu bora na za kisasa za uchimbaji na uchakataji madini, utunzaji wa mazingira, pamoja na kuanzisha mfumo wa masoko ya madini katika mikoa yote yenye madini ya metali na vito yaani metallic minerals and gemstones.

 

 

 

 

 

 

 

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

UCHUMI WA TANZANIA WAZIDI KUKUA NA KUIMARIKA

Hali ya uchumi wa Tanzania yazidi kuimarika na kukua  kwa asilimia 6.9 ikiwa ni  takwimu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.